The House of Favourite Newspapers

Lissu: Sitaki Huruma ya Mahakama, Nataka Haki ya Kikatiba – Video


Dar es Salaam, Julai 15, 2025 – Kesi ya uhaini inayomkabili mwanasiasa na wakili maarufu nchini, Tundu Antiphas Lissu, inatarajiwa kuendelea leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Antipas Lissu, amesema wazi kuwa hategemei huruma ya Mahakama bali anataka taratibu na haki za kikatiba zizingatiwe ipasavyo katika kesi inayomkabili.

Akizungumza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, Lissu amelalamikia ucheleweshwaji wa kesi unaofanywa na upande wa Jamhuri, akiutaja kuwa ni “uchezeaji wa utaratibu wa Mahakama” unaofanywa na Mawakili wa Serikali pamoja na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).

“Hoja yangu ni kwamba Mawakili wa Serikali na DPP wanachezea utaratibu wa Mahakama… Hii ni kinyume na wajibu wao wa kikatiba,” alisema Lissu kwa msisitizo, akionesha kuchoshwa na mfululizo wa maahirisho.

Lissu alifikishwa mahakamani Aprili 10, 2025 kwa shtaka la uhaini linalodaiwa kutendeka Aprili 3, 2025, ambapo inadaiwa alihamasisha kuzuia uchaguzi mkuu ujao. Kwa mujibu wa sheria, shtaka hilo halina dhamana, na kwa sasa anaendelea kushikiliwa mahabusu huku kesi hiyo ikisikilizwa mubashara kupitia kurasa rasmi za Mahakama.

Mbali na kesi hiyo, Lissu pia anakabiliwa na kesi nyingine ya kuchapisha taarifa za uongo, ambayo kwa sasa imekwama baada ya Mahakama Kuu kutupilia mbali maombi yake aliyowasilisha kupitia Masjala Ndogo ya Dar es Salaam.

Wakati mchakato wa kisheria ukiendelea, Lissu amesisitiza kuwa haki si zawadi inayotolewa kwa kuombewa huruma, bali ni haki ya msingi inayopaswa kutolewa kwa kila raia kwa mujibu wa Katiba.

Comments are closed.