IKIWA imebaki wiki moja kuanza kwa Ligi Kuu Bara, beki wa kati wa Simba, Method Mwanjali, amefunguka kuwa hatarajii kupata upinzani mkali kutoka kwa washambuliaji wa timu za ligi kutokana na kuamini uwezo wake ni mkubwa zaidi yao akiwemo Donald Ngoma wa Yanga.
Mwanjali ambaye ni raia wa Zimbabwe sawa na Ngoma, ni miongoni mwa wachezaji wanaofanya vizuri katika kambi ya Simba mkoani Morogoro kwa kuweza kulishawishi benchi la ufundi la timu hiyo linaloongozwa na kocha Mcameroon, Joseph Omog.
Akizungumza na Championi Ijumaa, Mwanjali alisema kuwa sababu kubwa iliyompeleka Simba ni kuisaidia kupata mataji mengi zaidi na siyo kupata upinzani kutoka kwa washambuliaji wa timu ambazo watakutana nazo kwenye ligi hiyo.
“Hawana nafasi ya kuniumiza kichwa kwa sababu kilichonileta Simba ni kitu kimoja, ni kuweza kuisaidia kubeba makombe na kushiriki mashindano makubwa, sasa hao kwangu lazima watakuwa ni wa kawaida,” alisema Mwanjali.
