
WAKATI leo tarehe 1 Disemba, 2021 ikiwa ni siku ya maadhimisho ya UKIMWI duniani ambayo kitaifa mwaka huu yanafanyika jijini Mbeya, Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) imetoa kiasi cha Sh milioni 84 kwa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS) ikiwa ni mchango wa kampuni kusaidia juhudi za serikali katika kupambana dhidi ya VVU na UKIMWI.
Akizungumza katika Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani jijini Mbeya, Makamu wa Rais wa GGML anayeshughulikia miradi endelevu, Simon Shayo amesema kaulimbiu ya mwaka huu isemayo “Zingatia Usawa. Tokomeza UKIMWI. Tokomeza Magonjwa ya Mlipuko,”ni muhimu kwa jamii mkoani Geita na Tanzania kwa ujumla.

Amesema Kampuni ya GGML kupitia kampeni ya GGML Kili Challenge imeendelea kushirikiana na watoa wachangiaji wengine kukabiliana na janga la UKIMWI.
“Haya yote yanafanyika kupitia utoaji wa huduma zinazozingatia usawa, zinazozingatia utu na haki kwa wale wote wanaonufaika na kampeni hii hasa walio katika mazingira magumu zaidi,” amesema.
Hata hivyo, katika maadhimisho hayo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, aliipatia GGML ngao na cheti kwa kutambua mchango wa kampuni hiyo katika mapambano dhidi ya VVU pamoja na mchango kuelekea siku ya Ukimwi Duniani.

Shayo amepokea cheti na ngao hiyo kwa niaba ya kampuni baada ya Mkurugenzi wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi, Dk. Leonard Maboko kumuomba waziri mkuu kutambua mchango wa wadau waliofanikisha maadhimisho hayo pamoja na kuendeleza juhudi za mapambano dhidi ya Ukimwi na VVU.
GGML Kili Challenge ni mpango wa kuchangisha pesa kwa ajili ya mapambano dhidi ya VVU ambapo kila mwaka kampuni kupitia mpango huo huandaa safari ya kupanda Mlima Kilimanjaro kwa njia ya kawaida na baiskeli.
Timu ya wapanda mlima hupanda hadi kufika kilele cha Uhuru huku timu ya waendesha baiskeli wakizunguka chini ya mlima huo.
Kilimanjaro Challenge ilizinduliwa miaka 20 iliyopita kwa lengo la kuongeza uelewa juu ya janga la Virusi Vya Ukimwi (VVU) na UKIMWI na kutoa msaada wa kifedha katika mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI. Tangu wakati huo, zaidi ya watu 800 kutoka sehemu mbalimbali duniani wameshiriki.

Kilimanjaro Challenge imeshirikiana na makampuni ya ndani na nje ya nchi na watu binafsi kutoka sehemu mbalimbali duniani na kufanikiwa kukusanya zaidi ya Sh bilioni 1.3 zilizonufaisha zaidi ya mashirika na asasi za kiraia (NGOs) 40 nchini.
Kampuni ya Geita Gold Mining Limited na TACAIDS, chini ya mwamvuli wa Kilimanjaro Challenge, wanatekeleza jukumu la kuongeza uelewa kuhusu janga la VVU na UKIMWI na wanaamini siku moja Tanzania itatangaza kumalizika kwa maambukizi ya VVU na UKIMWI.
NA MWANDISHI WETU

