Shilole Arudisha Huduma ya Shishifood Dar, Awasamehe Waliochoma Mgahawa Wake – Video

Baada ya kutangaza kurejesha huduma ya Shishifood kwa njia ya delivery ndani ya mkoa wa Dar es Salaam, Mwanamuziki na muigizaji wa filamu Bongo, Zuwena Mohamed ‘Shilole’ amefunguka na kusema kuwa amewasamehe vijana waliohusika kuchoma mgahawa wake ulioharibiwa Oktoba 29, 2025.
Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam, Shilole amesema licha ya tukio hilo kumuumiza kibiashara na kihisia, ameamua kuweka mbele msamaha, amani na kuangalia mustakabali wa biashara yake badala ya kuendelea kubeba chuki.
“Tukio lilikuwa gumu, lakini nimeamua kusamehe. Maisha yaendelee na kazi iendelee,” amesema Shilole.
Ni majuma kadhaa sasa yamepita tangu mgahawa wake kuteketezwa kwa moto, tukio lililosababisha kusitishwa kwa huduma kwa wateja wa Dar es Salaam. Hata hivyo, Shilole amesema amejipanga kurejea taratibu sokoni kwa kuanza na huduma ya kupeleka chakula kwa wateja walipo (delivery).
Ametangaza kuwa huduma hiyo itaanza kesho, Desemba 19, 2025, huku akiwahakikishia wateja wake kuwa ubora wa chakula na huduma utaendelea kuwa ule ule waliouzoea.
Hatua ya Shilole kurejesha huduma imepokelewa kwa furaha na mashabiki pamoja na wateja wake, wengi wakimpongeza kwa moyo wa msamaha, uthubutu na ujasiri wa kuendelea kusimama baada ya changamoto kubwa.
Shilole ni miongoni mwa wasanii wa Tanzania waliofanikiwa kuunganisha sanaa na biashara, hususan katika sekta ya chakula, kupitia brand ya Shishifood ambayo imepata umaarufu mkubwa jijini Dar es Salaam.

