Magori Afunguka: Simba Haijayumba Kama Inavyosemwa, Kelele Zinakuzwa – Video

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Klabu ya Simba SC, Crescentius Magori, amevunja ukimya na kueleza sababu zilizochangia kuyumba kwa kiwango cha timu katika baadhi ya michezo ya hivi karibuni, akisisitiza kuwa hali halisi haiko mbaya kama inavyotafsiriwa na baadhi ya wadau wa soka.
Akizungumza kuhusu changamoto za kiufundi, Magori amesema mabadiliko ya benchi la ufundi yalikuwa sababu kubwa ya kuyumba kwa muda kwa timu hiyo.
“Kiufundi timu iliyumba kwa sababu kocha aliyeanza msimu na timu aliondoka, akaja kocha ambaye hatukukubaliana. Hilo ni jambo ambalo haliepukiki katika mpira,” amesema Magori.
Ameongeza kuwa majeruhi ya wachezaji muhimu yamekuwa yakipuuzwa kwenye mijadala ya mashabiki na wachambuzi, huku lawama zikielekezwa zaidi kwenye matokeo.
“Kitu kingine ambacho watu hawakisemi ni kwamba kwenye mechi ya Ngao ya Jamii beki muhimu wa kati aliumia, mechi iliyofuata kipa namba moja aliumia. Tukiwa Mali, beki mwingine muhimu wa kati naye aliumia,” ameongeza.
Kwa mujibu wa Magori, licha ya changamoto hizo, matokeo ya Simba SC kwenye Ligi Kuu bado ni ya kuridhisha.
“Tumecheza mechi tano za ligi na tumepoteza mechi moja tu, lakini kelele zinazopigwa ni kama mwisho wa dunia,” amesema.
Kuhusu matarajio ya mashindano ya kimataifa, Magori amekiri kuwa kushindwa kufuzu hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ni jambo lisilopendeza, lakini si la kipekee kwa Simba SC pekee.
“Tusipoingia robo fainali ya Ligi ya Mabingwa ni jambo baya, hatukusudia, lakini mwaka jana kuna timu haikuingia robo fainali mlipiga kelele?” amehoji.

