Waziri Mkuu Mstaafu Majaliwa Aagwa kwa Heshima Kubwa Ruangwa

Jumamosi Desemba 20, 2025, wananchi wa Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi wameandaa hafla maalum ya kumshukuru na kumuaga aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Ruangwa na Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa.
Hafla hiyo imefanyika katika Uwanja wa Wandolwa, Ruangwa Mjini, ikihudhuriwa na maelfu ya wananchi, viongozi wa Serikali, Chama cha Mapinduzi (CCM), viongozi wa dini pamoja na makundi mbalimbali ya kijamii kutoka ndani na nje ya wilaya hiyo.

Akizungumza katika hafla hiyo, Kassim Majaliwa aliwashukuru wananchi wa Ruangwa kwa imani kubwa waliyoendelea kumuonyesha kwa miaka yote aliyowawakilisha bungeni na kuhudumu katika nafasi mbalimbali za uongozi wa kitaifa. Alisema mafanikio aliyoyapata yalitokana na ushirikiano mkubwa wa wananchi, viongozi na watumishi wa umma.
“Nimekuwa kiongozi kwa sababu ya nyinyi. Ushirikiano wenu ndio ulionipa nguvu ya kutumikia taifa kwa uaminifu na uzalendo,” alisema Majaliwa.
Kwa upande wao, wananchi na viongozi waliopata fursa ya kuzungumza walimsifu Majaliwa kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya Ruangwa, ikiwemo uboreshaji wa miundombinu ya barabara, elimu, afya, maji pamoja na kukuza mshikamano wa kijamii.
Hafla hiyo pia ilipambwa na burudani mbalimbali, ngoma za asili na hotuba za shukrani, huku wananchi wakionyesha hisia za upendo, heshima na shukrani kwa kiongozi wao aliyewatumikia kwa muda mrefu.


