Gabon Yaondoa Adhabu Dhidi ya Aubameyang na Timu ya Taifa

Shirikisho la Soka la Gabon limetangaza kufuta hatua zote zilizokuwa zimechukuliwa dhidi ya timu ya taifa pamoja na baadhi ya wachezaji wake, akiwemo nahodha Pierre-Emerick Aubameyang, kufuatia kuondolewa mapema kwenye michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika 2025.
Katika michuano hiyo inayoendelea nchini Morocco, Gabon ilipoteza mechi zote za Kundi F dhidi ya Cameroon, Msumbiji na Côte d’Ivoire, hali iliyosababisha hasira kubwa kwa viongozi wa serikali.
Baada ya matokeo hayo, Waziri wa Michezo wa Gabon, Paul Ulrich Kessany, alitangaza kupitia televisheni ya taifa kuwa timu ya taifa imesimamishwa, pamoja na kuchukuliwa hatua dhidi ya Aubameyang na beki Bruno Ecuele Manga.
Hata hivyo, Shirikisho la Soka la Gabon sasa limethibitisha kufuta maamuzi hayo, likisema hatua hizo zingeiweka nchi katika hatari ya kusimamishwa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) kutokana na kuingilia kisiasa masuala ya soka.
Shirikisho hilo limeeleza kuwa kipaumbele chake kikuu sasa ni maandalizi ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika 2027, yatakayofanyika kwa pamoja nchini Tanzania, Uganda na Kenya.

