The House of Social Media
gunners X

Mmoja Afariki, 12 Wajeruhiwa Ajali ya Lori na Basi Shinyanga – Video

0

Mtu mmoja amefariki dunia na wengine 12 kujeruhiwa katika ajali ya barabarani iliyohusisha roli na basi, iliyotokea leo Januari majira ya saa 12:30 asubuhi katika eneo la Mnada wa Tinde, wilayani Shinyanga.

Marehemu ni dereva wa roli Hitayezu Elias (35), lenye namba za usajili RAE 849 N kutoka nchini Rwanda, ambaye alikuwa amebeba shehena ya mchele.

Ajali hiyo ilihusisha basi la Kampuni ya Kisire lenye namba za usajili T 229 EEL, lililokuwa likisafiri kutoka Kahama kwenda Mwanza.

Akizungumza na vyombo vya habari katika eneo la tukio, Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi, alisema kuwa basi hilo lilikuwa likiendeshwa kwa mwendokasi, na lilipofika katika mnada wa Tinde liligonga toroli la matikiti kabla ya kugongana uso kwa uso na roli hilo.

Alisema basi hilo lilikuwa na jumla ya abiria 42, ambapo 12 walijeruhiwa, kati yao, watano hali zao ni mbaya na wamepelekwa Hospitali ya Rufaa Mwawaza, huku wengine saba wakipatiwa matibabu katika Zahanati ya Tinde.

“Chanzo cha ajali hii ni uzembe wa dereva wa basi la Kisire ambaye hakuchukua tahadhari. Baada ya ajali kutokea alikimbia, na Jeshi la Polisi linaendelea kumsaka ili achukuliwe hatua za kisheria,” alisema Kamanda Magomi.

Kwa upande wake, mmoja wa majeruhi, Robert Daudi, alisema alikuwa akisafiri na watoto wake watatu, na kwamba waliposikia kishindo kikubwa ndipo waligundua kuwa wamepata ajali, hata hivyo watoto wake wako salama.

 

 

Leave A Reply