Sean ‘Diddy’ Combs Aomba Huruma ya Jaji Kabla ya Hukumu
Sean ‘Diddy’ Combs amemuandikia barua ya kuomba huruma Jaji Arun Subramanian aliyesimamia kesi yake, siku moja kabla ya kuhukumiwa, baada ya kupatikana na hatia mwezi Julai kwa makosa mawili ya kusafirisha watu kwa ajili ya kushiriki katika ukahaba.
Hukumu ya Diddy inatarajiwa kutolewa leo Ijumaa, Oktoba 3, 2025 baada ya kukutwa na hatia katika makosa mawili kati ya makosa kadhaa yaliyokuwa yakimkabili.
“Nilipotea njia. Nilipotea katika safari yangu. Nikapotelea kwenye dawa za kulevya na starehe kupita kiasi. Anguko langu lilitokana na ubinafsi wangu. Nimewekwa chini na kuvunjwa kabisa moyoni mwangu,” aliandika Combs, akiongeza:
“Mimi wa zamani nilikufa gerezani na toleo jipya langu likazaliwa upya. Gereza litakubadilisha au litakuua—mimi nimechagua kuishi.”
Katika barua hiyo aliyoiandika jana Alhamisi, Combs alimuomba Jaji Subramanian amruhusu awe “mfano wa kile mtu anaweza kufanya endapo atapewa nafasi ya pili.”
Combs amekuwa gerezani jijini Brooklyn, New York tangu alipokamatwa Septemba, 2024 na anakabiliwa na kifungo cha hadi miaka 10 jela kwa kila kosa alilopatikana nalo na hatia.
Kesi dhidi yake iliendeshwa kwa muda wa miezi miwili katika mahakama ya Manhattan msimu wa kiangazi.
“Ninatambua kwamba kesi hii imepata ufuatiliaji mkubwa wa vyombo vya habari duniani kote na Mheshimiwa Jaji unaweza kushawishika kuniweka mfano,” aliandika Combs.
“Ningekuomba mheshimiwa Jaji unifanye mfano wa kile mtu anaweza kufanya akipewa nafasi ya pili.”