Macron Amrejesha Sébastien Lecornu Kama Waziri Mkuu wa Ufaransa

Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, amemteua tena Sébastien Lecornu kuwa Waziri Mkuu, hatua iliyowashangaza wengi baada ya kiongozi huyo kujiuzulu mapema wiki hii.
Taarifa iliyotolewa na Ikulu ya Élysée tarehe 10 Oktoba 2025 imesema:
“Rais wa Jamhuri amemteua Bw. Sébastien Lecornu kuwa Waziri Mkuu na kumkabidhi jukumu la kuunda Serikali.”
Uamuzi huo umetafsiriwa na wachambuzi kama ishara ya jitihada za Macron kuimarisha uthabiti wa kisiasa katika kipindi ambacho taifa hilo linakabiliwa na mgawanyiko mkubwa wa kisiasa bungeni.
Hata hivyo, upinzani umeikosoa vikali hatua hiyo, ukidai kuwa uteuzi wa Lecornu hautaleta mabadiliko yoyote makubwa kwani amekuwa sehemu ya serikali zilizopita. Wanasiasa wa upinzani wamesema wananchi wanatarajia sura mpya na dira tofauti badala ya kurudia viongozi wale wale.
Ufaransa kwa sasa inapitia kipindi kigumu cha kisiasa ambacho hakijawahi kushuhudiwa kwa miaka ya karibuni, huku serikali ikikabiliana na changamoto za kiuchumi, maandamano ya kijamii na upungufu wa uungwaji mkono kwa Rais Macron.