Rais Samia: Bilioni 200 zimetengwa kuwawezesha vijana, Serikali yaja na Wizara Maalumu ya Vijana

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Samia Suluhu Hassan, amesema serikali ya awamu ya sita imetenga kiasi cha shilingi bilioni 200 kwa ajili ya kuwawezesha vijana kujikwamua kiuchumi kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo.
Akizungumza Novemba 14, 2025 Rais Samia alisema hatua hiyo ni sehemu ya mkakati mpana wa serikali kuhakikisha vijana wanapata mtaji, maarifa na mazingira rafiki ya kuanzisha au kukuza shughuli zao za kiuchumi.
Aidha, Rais Samia ametangaza kuwa serikali imeamua kuanzisha Wizara kamili ya Vijana, ambayo itakuwa mahsusi kushughulikia changamoto, fursa na maendeleo ya vijana nchini. Wizara hiyo itasimamia sera, programu na mikakati ya kuwawezesha vijana katika nyanja za ajira, ubunifu, biashara na teknolojia.
Vilevile, Rais Samia amesema anafikiria kuanzisha kitengo maalumu ndani ya Ofisi ya Rais ambacho kitakuwa kinamshauri moja kwa moja kuhusu masuala ya vijana, ili kuhakikisha maamuzi ya serikali yanawagusa moja kwa moja na kwa ufanisi.

