Dkt. Mwigulu Ahimiza Haki kwa Watanzania, Afungua Maadhimisho Ya Wiki Ya Usafiri Endelevu Ardhini

WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba leo Novemba 26, 2025 amefungua Maadhimisho ya Wiki ya Usafiri Endelevu Ardhini Mwaka 2025 yanayofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza mbele ya wajumbe wa mkutano, Dkt. Mwigulu alisema kuwa hata awe Waziri Mkuu kwa muda mfupi, hataruhusu Watanzania kugawanywa kwa madaraja.
“Nimemsikia mwanaharakati mmoja akisema huyu ndiye atakayekuwa Waziri Mkuu wa muda mfupi zaidi. Sawa! Hata niwe Waziri Mkuu kwa wiki moja, sitaruhusu Tanzania iwe nchi ya mabwana na watwana,” alisema Dkt. Mwigulu.
Waziri Mkuu aliongeza kuwa siwezi kuruhusu sheria isiyo ya haki ambapo wa daraja la chini wanadhibitiwa palepale kwa makosa, huku wa daraja la juu wakidumu bila kadhia.
“Kuna sheria imetungwa kuwalinda wa daraja la juu na kuwatweza wa daraja la chini. Akikosea wa daraja la chini anaadhibiwa mara moja, na wa daraja la juu analindwa na kupita tu,” alisema.
Aidha, Dkt. Mwigulu aliweka wazi kuwa atawapigania wa kawaida, kwa sababu hao ndio atakaoishi nao, na hata akifa, hao ndio watakaomzika.
“Nitawasemea wale wa daraja la chini kwa sababu hata nikitoka, hao ndio nitakaoishi nao. Na hata nikifa, hao ndio watakaonizika,” alisisitiza.
Hotuba yake imepokelewa kwa shangwe na wanahabari, huku ikionesha dhamira yake ya kuhakikisha usawa, haki, na heshima kwa Watanzania wote, bila kujali hali yao ya kiuchumi au kijamii.


