Trump Acharuka Baada ya Shambulio kwa Wanajeshi karibu na Ikulu ya White House

Wanajeshi wawili wa Ulinzi wa Kitaifa (National Guard) wamejeruhiwa vibaya baada ya kushambuliwa kwa risasi karibu na Ikulu ya White House jijini Washington DC, katika tukio ambalo meya wa jiji hilo amelielezea kama “shambulio la kulengwa”.
Tukio hilo lilitokea Jumatano alasiri, wakati mshukiwa mmoja alipojitokeza na kuwafyatulia risasi walinzi hao waliokuwa doria katika eneo hilo. Kwa mujibu wa maafisa wa polisi, milio ya risasi ilisababisha taharuki kubwa na kupelekea walinzi wengine wa Ulinzi wa Kitaifa waliokuwa karibu kumzingira mshukiwa huyo na hatimaye kumkamata.
Mshambuliaji Akamatwa Akiwa Amejeruhiwa
Vyanzo vya utekelezaji wa sheria viliiambia CBS News kuwa mshukiwa huyo alipigwa risasi mara nne wakati wa kumdhibiti. Alitambulika kama Rahmanullah Lakanwal, raia wa Afghanistan mwenye umri wa miaka 29, ambaye aliingia Marekani mwaka 2021.

Hadi kufikia Jumatano usiku, vyanzo hivyo vilisema mshukiwa hakuwa akishirikiana na mahojiano ya polisi, huku uchunguzi ukiendelea kubaini nia ya shambulio lake. Bado haijafahamika ni aina gani ya silaha aliyotumia.
Wanajeshi Wawili Hali Mbaya
Walinzi wawili wa National Guard waliojeruhiwa na kupelekwa hospitali wakiwa katika hali mbaya. Maafisa hawakutaja majina yao, lakini walisema walikuwa kwenye jukumu la ulinzi wa eneo la serikali lililokuwa na ulinzi mkali.
Rais wa Marekani, Donald Trump, ambaye wakati tukio linatokea alikuwa jimboni Florida, alitoa taarifa kali akisema shambulio hilo ni “kitendo cha ugaidi” kilichofanywa na mtu aliyeingia nchini kupitia mpango wa uhamiaji katika utawala wa aliyemtangulia, Joe Biden.
“Mshukiwa atalipa gharama kubwa zaidi kwa kitendo hiki cha kigaidi,”alisema Rais Trump katika hotuba ya moja kwa moja Jumatano usiku.
Rais huyo pia aliitisha uchunguzi mpya wa raia wote wa Afghanistan walioingia Marekani kuanzia mwaka 2021, akidai kuwa ni muhimu kufanya tathmini upya ya usalama wao.


