The House of Favourite Newspapers
gunners X

Video: Jeshi la Polisi Laanza Uchunguzi Dhidi ya Kauli ya OCD Chunya

0

Jeshi la Polisi Tanzania limesema linafanya uchunguzi kuhusu taarifa inayoenea kwenye mitandao ya kijamii ikidaiwa kutolewa na Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD) wa Chunya mkoani Mbeya, inayomwonesha akitoa maelekezo kwa wamiliki wa vituo vya mafuta.

Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa Novemba 26, 2025 na Msemaji wa Polisi Makao Makuu Dodoma, DCP David Misime, imeelezwa kuwa OCD hana mamlaka ya kuitisha waandishi wa habari na kutoa taarifa kwao, hivyo chanzo na uhalali wa taarifa hiyo vinachunguzwa.

Katika taarifa hiyo, Jeshi la Polisi limesema limechukua hatua za haraka kufuatilia video na maelezo yanayosambaa mtandaoni ili kubaini ukweli wake, likisisitiza kuwa taratibu rasmi lazima zifuatwe katika utoaji wa taarifa za kiusalama.

“Uchunguzi huo unafanyika ili kupata ukweli wa taarifa hiyo, kwani hana mamlaka ya kuita waandishi wa habari na kutoa taarifa kwao. Ikibainika hivyo hatua stahiki zitachukuliwa mara moja”, ameeleza Misime.

Hata hivyo, tukio lililosababisha taarifa hiyo kuibuka linahusiana na maelekezo yaliyotolewa mapema na Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Chunya, SSP Nestory John, aliyewaonya wauzaji wa mafuta kutowauzia madereva wa bodaboda mafuta yanayozidi lita moja kuelekea Desemba 9.

Alisema wale wanaouza mafuta kwenye vidumu na wanaoendesha biashara kwa njia isiyo rasmi wataendelea kufuatiliwa ili kudhibiti matumizi mabaya ya bidhaa hiyo, kutokana na taarifa za uwezekano wa kampeni ya maandamano siku hiyo—hatari ambayo inaweza kuchochea vitendo vya uvunjifu wa amani, ikiwemo kuchomewa vituo vya mafuta.

Akizungumza na waandishi wa habari, SSP John alisema ushirikiano kati ya wananchi na vyombo vya usalama ni msingi muhimu wa kudumisha amani wilayani humo. Alisisitiza umuhimu wa vituo vya mafuta kufunga kamera za CCTV ili kuimarisha ufuatiliaji wa matukio ya kiusalama na kuboresha utambuzi wa vitendo vya hatari kwa wakati.

 

Leave A Reply