Kiongozi wa wanamgambo Darfur afungwa miaka 20 na ICC

Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC), imemhukumu kiongozi wa wanamgambo wa Janjaweed nchini Sudan Ali Kushayb kifungo cha miaka 20 jela, kwa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu. Uhalifu huu ulifanywa wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe miaka ishirini iliyopita katika jimbo la Darfur magharibi mwa Sudan.
Ni mbabe wa kwanza wa kivita wa Sudan kuhukumiwa na ICC.
Ali Mohamed Ali Abd-Al-Rahman, anayejulikana pia kwa jina lake la kivita Ali Kushayb, alipatikana na hatia mnamo mwezi Oktoba 2025 kwa makosa mengi dhidi ya ubinadamu na uhalifu wa kivita, ikiwa ni pamoja na ubakaji, mauaji, na mateso yaliyofanywa kati ya mwaka 2003 na 2004 katika jimbo la Darfur, magharibi mwa Sudan.
Mwendesha mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu aliomba kifungo cha maisha jela: majaji wa ICC walitangaza siku ya Jumanne, Desemba 9, 2025, kifungo cha miaka 20 jela. Kutoka kwa hukumu hii, miaka mitano ambayo tayari ametumikia kizuizini kabla ya kesi tangu kujisalimisha kwake kwa Mahakama mnamo mwezi Juni 2020 itapunguzwa kwenye miaka hiyo 20 aliyohukumiwa.

