M23 Watangaza Kujiondoa Uvira kwa Masharti, Wadokeza Shinikizo la Marekani

Kundi la waasi la M23 limetangaza kujiondoa katika Mji wa Uvira, Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), kwa masharti maalumu, likidai hatua hiyo inalenga kupunguza mvutano wa kijeshi na kuonyesha utayari wake wa kushiriki katika juhudi za amani.
Taarifa ya uamuzi huo imetolewa usiku wa Desemba 15 kuamkia Desemba 16, ikieleza kuwa kujiondoa huko ni matokeo ya shinikizo kutoka kwa Marekani.
M23 ilichukua udhibiti wa Uvira mwanzoni mwa Desemba 2025, wakipata mafanikio ya kijeshi katika eneo hilo kabla ya kutangaza kujiondoa.
Katika masharti yao, M23 wametaka jeshi la DRC liondoke Uvira, raia walindwe kikamilifu, na kuwepo kwa kikosi cha kimataifa au kisichoegemea upande wowote cha kufuatilia utekelezaji wa usitishaji mapigano.
Kundi hilo limesisitiza kuwa masharti hayo ni muhimu ili kuhakikisha usalama wa raia na kuepuka mapigano mapya baada ya wao kuondoka.
M23 imeeleza kuwa Marekani imekuwa ikiongeza shinikizo kwa Rwanda, ambayo mara nyingi hutuhumiwa kuunga mkono kundi hilo, ili ipunguze msaada wa kijeshi na kisiasa.
Ingawa M23 imekuwa ikipata mafanikio ya kijeshi katika wiki za hivi karibuni, viongozi wake wamesema kujiondoa kwao ni hatua ya kujenga imani na kuunga mkono mchakato wa amani wa Doha, unaolenga kufikia suluhu ya kudumu kwa mgogoro wa Mashariki mwa DRC.
Hatua hiyo imekuja wakati Rais wa DRC, Félix Tshisekedi, akifanya ziara ya kidiplomasia nchini Angola ambako alikutana na Rais João Lourenço, mpatanishi mkuu wa mchakato wa Luanda.
Mazungumzo yao yalilenga kuimarisha juhudi za kikanda na kimataifa za kusitisha mapigano, kupunguza mvutano kati ya DRC na Rwanda, pamoja na kuhakikisha makubaliano ya amani yanatekelezwa kwa vitendo.
Tshisekedi amesisitiza kuwa kujiondoa kwa masharti hakupaswi kuzuia serikali ya DRC kurejesha udhibiti kamili wa maeneo yake, huku akitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuendelea kushinikiza M23 na Rwanda kushiriki kwa dhati katika mazungumzo ya amani.

