The House of Favourite Newspapers
gunners X

Rais Samia Akabidhiwa Tuzo Tatu za Utalii Kimataifa – Picha

0

Rais Samia Suluhu Hassan, amepokea tuzo tatu za kimataifa za utalii zilizotolewa na Taasisi ya World Travel Awards (WTA), katika hafla iliyofanyika Ikulu Ndogo ya Tunguu, Zanzibar, leo Januari 5, 2026.

Akizungumza na viongozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii kabla ya kupokea tuzo hizo, Rais Samia aliipongeza sekta ya utalii kwa kuendelea kuitangaza Tanzania kimataifa na kuifanya kuwa miongoni mwa nchi vinara wa utalii barani Afrika na duniani kwa jumla.

Miongoni mwa tuzo zilizopokelewa ni ile ya Tanzania kutangazwa kuwa Eneo Bora la Utalii wa Safari Duniani (World’s Leading Safari Destination), tuzo aliyokabidhiwa Rais Samia na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji.

Aidha, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti imetunukiwa tuzo ya Hifadhi Bora Duniani (World’s Leading National Park), hatua inayozidi kuimarisha hadhi ya Tanzania kama kitovu cha utalii wa asili na uhifadhi.

Baada ya kupokea tuzo hizo, Rais Samia alipiga picha ya pamoja na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji, pamoja na Naibu Waziri wa wizara hiyo, Hamad Hassan Chande, huku akisisitiza umuhimu wa kuendelea kuwekeza katika uhifadhi, huduma bora kwa watalii na utangazaji wa vivutio vya utalii.

Tuzo hizo zimetolewa na Taasisi ya World Travel Awards yenye makao makuu yake jijini London, Uingereza, na zinatambua mchango wa Tanzania katika kukuza na kuendeleza utalii kwa viwango vya juu kimataifa.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akionesha Tuzo ambayo Hifadhi ya Serengeti imeshinda kuwa Hifadhi bora Duniani (World’s Leading National Park, Ikulu ndogo ya Tunguu Zanzibar tarehe 05 Januari, 2026. Tuzo hiyo imetolewa na Taasisi ya World Travel Awards (WTA) yenye Makao Makuu yake Jijini London, Uingereza.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha na Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji pamoja na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Hamad Hassan Chande mara baada ya kupokea Tuzo 3 za Utalii za “WORLD TRAVEL AWARDS” ambazo Tanzania imeshinda, Ikulu Ndogo Tunguu, Zanzibar tarehe 05 Januari, 2026.

Leave A Reply