Wananchi Arusha waeleza machungu ya Oktoba 29 mbele ya Tume ya Uchunguzi

Baadhi ya wananchi mkoani Arusha wameieleza Tume ya Uchunguzi wa Matukio ya Oktoba 29, 2025 changamoto mbalimbali walizokumbana nazo wakati na baada ya vurugu na maandamano yaliyotokea siku hiyo.
Wananchi hao wameyasema hayo Januari 5, 2026 mkoani Arusha mbele ya Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Mkuu Mstaafu wa Tanzania, Mohammed Chande. Wameeleza athari kubwa zilizowakumba ikiwemo kupoteza wapendwa wao, huku wengine wakidai hadi sasa hawajui walipo ndugu zao.
Mmoja wa wananchi walioathirika amesema alimpoteza mtoto wake katika matukio hayo, ambapo kama familia walizunguka hospitali mbalimbali jijini Arusha ikiwamo Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru wakisaka mwili wa mtoto wao bila mafanikio. Ameeleza kuwa walichofanikiwa kukipata ni kiatu cha mtoto wao, hali iliyowafanya wakate tamaa ya kumuona tena hadi leo.
Kwa upande wake, Humphrey Thomas mkazi wa Sombetini mkoani Arusha, amehoji sababu zilizosababisha vijana kuandamana tarehe 29 Oktoba, akisema matukio hayo yalikuwa na pande mbili—waliokuwa waandamanaji na wasiokuwa waandamanaji. Ameeleza kuwa wengi wa walioathirika hawakushiriki maandamano hayo.
Akisisitiza hoja yake, Humphrey amesema mtoto wake hakuwa mwandamanaji lakini alipigwa risasi. “Mimi ndo baba ya aliyepigwa risasi hapa Arusha mjini, mtoto alitoka kufuata mahitaji yake lakini wakati anarudi nyumbani alipigwa risasi,” amesema Humphrey.
Hata hivyo, ameiomba tume hiyo kutofautisha kati ya waathirika wa maandamano na wananchi wasiokuwa waandamanaji, akisisitiza kuwa si sahihi kuwaita waathirika wote kuwa ni waandamanaji pekee.
Mwenyekiti wa Tume ya Uchunguzi wa Matukio ya Oktoba 29, 2025, Jaji mstaafu Mohammed Chande amesema hakuna mtu anayeweza kueleza kwa undani kilichotokea mkoani Arusha zaidi ya wananchi walioathirika wenyewe. Amesema lengo la tume hiyo ni kusikiliza, kuchambua na kufanyia kazi maelezo ya waathirika pamoja na mashuhuda wa matukio hayo.
Jaji Chande ameongeza kuwa kama tume lazima wafahamu chanzo cha yaliyotokea, akisisitiza kuwa Tanzania imekuwa nchi ya amani tangu uhuru na matukio ya Oktoba 29 hayakuwa yakitarajiwa.
Stori na Elvan Stambuli, Global

