The House of Favourite Newspapers
gunners X

Halmashauri ya Wilaya ya Buchosa Yatangaza Nafasi 08 za Ajira

0

Halmashauri ya Wilaya ya Buchosa imetangaza nafasi nane (08) za ajira kwa Watanzania wenye sifa, kufuatia kibali kutoka Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Tangazo hilo limetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Buchosa kupitia kumbukumbu namba AB.03/117/01/LV II/18 ya tarehe 15 Januari, 2026, likieleza kuwa nafasi hizo zinahusisha kada mbalimbali ikiwemo Msaidizi wa Kumbukumbu, Dereva na Mwandishi Mwendeha Ofisi.

Kwa mujibu wa tangazo hilo, nafasi tano (05) ni za Msaidizi wa Kumbukumbu Daraja la II, ambapo majukumu yake ni pamoja na kuorodhesha barua zinazoingia na kutoka, kusambaza na kurejesha majalada, kufuatilia mzunguko wa majalada pamoja na kutunza kumbukumbu za taasisi. Waombaji wanatakiwa kuwa na elimu ya Kidato cha Nne au Sita na Stashahada (Diploma – NTA Level 6) ya Utunzaji wa Kumbukumbu pamoja na ujuzi wa matumizi ya kompyuta. Nafasi hizi zinalipwa kwa ngazi ya mshahara TGS C.

Aidha, nafasi mbili (02) zimetengwa kwa Dereva Daraja la II, ambapo majukumu yake ni kukagua gari kabla na baada ya safari, kuendesha watumishi kwenye safari za kikazi, kufanya matengenezo madogo, kuandika daftari la safari (log book) na kuhakikisha usafi wa gari. Waombaji wanatakiwa kuwa na elimu ya Kidato cha Nne, leseni ya Daraja C au E, uzoefu wa kuendesha gari kwa zaidi ya mwaka mmoja bila kusababisha ajali, pamoja na cheti cha mafunzo ya msingi ya udereva kutoka VETA au chuo kinachotambuliwa na Serikali. Nafasi hizi zinalipwa kwa ngazi ya mshahara TGS B.

Nafasi moja (01) imetengwa kwa Mwandishi Mwendeha Ofisi Daraja la II, mwenye jukumu la kuchapa nyaraka, kupokea na kuelekeza wageni, kutunza kumbukumbu za miadi na ratiba, kuandaa vikao na kusimamia majalada. Sifa zinazohitajika ni elimu ya Kidato cha Nne na Stashahada ya Uhazili au cheti cha NTA Level 6, pamoja na ujuzi wa hati mkato ya Kiswahili na Kiingereza kwa kasi ya maneno 100 kwa dakika moja na matumizi ya programu za kompyuta za ofisi. Nafasi hii inalipwa kwa ngazi ya mshahara TGS C.

SOMA ZAIDI HAPA >>>>NAFASI ZA KAZI HALMASHAURI YA WILAYA YA BUCHOSA 

Leave A Reply