The House of Social Media
gunners X

Simba Yawataka Mashabiki Kuungana Dhidi ya Esperance ya Tunisia

0

Semaji wa Simba Sports Club, Ahmed Ally, ametoa wito mzito kwa Wanasimba kuacha lawama na migawanyiko, akisisitiza kuwa huu ni wakati wa mshikamano na mapambano kwa ajili ya maslahi ya klabu hiyo kuelekea mchezo muhimu wa Jumapili dhidi ya Esperance ya Tunisia.

Akizungumza na Wanasimba kutoka Tawi la Wekundu wa Kurasini Mji Mpya, Semaji amesema Simba inahitaji kila Mwanasimba kusimama imara na kuipa nguvu timu, akieleza kuwa mafanikio yatakayopatikana yatakuwa ni heshima ya Simba Sports Club kwa ujumla.

“Lawama hazijawahi kujenga. Huu sio muda wa mpasuko, huu ni muda wa kuimba wimbo mmoja. Mechi ya Jumapili ipo mikononi mwetu na tukiamua Esperance atakuja Uwanja wa Benjamin Mkapa,” amesema Semaji.

Ameongeza kuwa Simba ina uzoefu mkubwa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ikiwa ni miongoni mwa waanzilishi wa mashindano hayo Tanzania, na kuzoea kufika hatua ya robo fainali mara kwa mara.

Semaji amesisitiza kuwa iwapo Simba itashindwa, basi si kiongozi wala CEO aliyeshindwa bali ni klabu nzima, jambo ambalo halipaswi kukubalika wakati timu ina uwezo wa kusonga mbele.

“Tusikubali tukaishia njiani. Tuingie kishujaa, Esperance anaweza kufungwa. Kazi ya kumfunga mwarabu sio ya wachezaji peke yao, ni kazi ya mashabiki,” alisisitiza.

Kuhusu hali ya timu, Semaji amesema Simba iliyocheza Tunisia imeonesha mabadiliko makubwa, akibainisha kuwa kosa dogo pekee ndilo liligharimu matokeo, huku akiahidi kuwa Jumapili mashabiki wataiona Simba iliyokamilika zaidi.

Pia ametangaza kuwa klabu inaendelea kuimarika kikosi chake kwa sajili mpya, akieleza kuwa baada ya kutangazwa kwa mchezaji mmoja, mwingine atasajiliwa rasmi kupitia wakala JayRutty.

“Kwa Mwanasimba yeyote kukata tamaa hivi sasa ni marufuku. Robo fainali bado ipo mikononi mwetu. Mnyama kufanya maajabu inawezekana,” alihitimisha Semaji.

Leave A Reply