Baada ya Kumng’oa Maduro, Trump Afungua Mlango wa Mazungumzo na Colombia

Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema atakutana na Rais wa Colombia, Gustavo Petro, katika Ikulu ya White House hivi karibuni, siku chache tu baada ya kutoa matamshi yaliyoashiria uwezekano wa operesheni ya kijeshi dhidi ya Colombia.
Tangazo hilo linakuja kufuatia operesheni ya kushtukiza ya kijeshi ya Marekani iliyofanyika mwishoni mwa wiki mjini Caracas, Venezuela, na kusababisha kukamatwa kwa Rais wa nchi hiyo, Nicolás Maduro. Hatua hiyo imezua mjadala mpana na wasiwasi mkubwa katika ukanda wa Amerika Kusini.
Serikali ya Venezuela imedai kuwa idadi ya watu walioumia katika operesheni hiyo ni kubwa zaidi kuliko ilivyotangazwa awali, ikisema kuwa zaidi ya watu 100 wamepoteza maisha. Ripoti za awali kutoka vyombo vya habari vya ndani zilieleza kuwa wanajeshi 23 wa Venezuela na 32 wa Cuba waliuawa wakati majeshi ya Marekani yalipovamia makazi ya Maduro.
Katika mazungumzo ya simu kati ya Trump na Petro, viongozi hao wawili walijadili changamoto za biashara ya dawa za kulevya pamoja na tofauti za kidiplomasia zilizopo kati ya mataifa yao.

Trump alimpongeza Petro kwa kile alichokiita “mtindo wake wa mazungumzo”, licha ya kuwa siku chache kabla alikuwa ametoa onyo kali dhidi yake.
Colombia inatajwa kuwa moja ya vituo muhimu vya biashara ya dawa za kulevya, hususan cocaine, pamoja na kuwa na utajiri mkubwa wa mafuta, madini na rasilimali nyingine, jambo linaloifanya kuwa nchi yenye uzito mkubwa kisiasa na kiuchumi katika eneo hilo.
Baada ya operesheni nchini Venezuela, Trump alitoa kauli kali dhidi ya Petro, hatua iliyomfanya Rais huyo wa Colombia kujibu kwa onyo akisema nchi yake haitakubali shinikizo wala vitisho vya kijeshi kutoka kwa taifa lolote.
Hata hivyo, baadaye Trump aliandika kwenye mtandao wake wa kijamii kwamba mazungumzo yao yalikuwa ya “heshima kubwa”, akiongeza kuwa Wizara za Mambo ya Nje za nchi hizo mbili zimeanza maandalizi ya ziara ya Rais Petro kwenda Washington.
Ikumbukwe kuwa Marekani iliwahi kuiwekea Colombia vikwazo mwaka jana, ikimtuhumu Rais Petro kushindwa kudhibiti usafirishaji wa dawa za kulevya, madai ambayo Petro amekuwa akiyakanusha, akisisitiza kuwa amepambana na biashara hiyo kwa miaka mingi.
Wakati huo huo, Venezuela imekosoa vikali hatua ya Marekani kumuondoa madarakani Rais Maduro, lakini imesema iko tayari kuendelea kushirikiana na Marekani katika sekta ya nishati, kwa maslahi ya pande zote.

