Boomplay Watoa Takwimu za Muziki 2020: Rayvanny, Zuchu Waongoza

App namba moja kwa huduma ya muziki Barani Afrika, Boomplay imemtaja msanii Rayvanny kuwa ndiyo mwanamuziki wa kiume aliyesikilizwa zaidi Tanzania huku Zuchu akiwa ndiyo mwanamuziki wa kike aliyesikilizwa zaidi Tanzania. Hii ni kwa mujibu wa taarifa na takwimu rasmi za muziki kwa mwaka 2020.

Taarifa hiyo iliyowekwa kwenye ripoti maalumu kuhusu muziki imeegemea zaidi kwenye data kutoka katika app hiyo ya muziki ambayo kwa mwezi ina wastani wa watumiaji milioni 50 ulimwenguni kote. Boomplay inajivunia kuwa na aina tofauti za nyimbo ambazo idadi yake ni zaidi ya milioni 44, ambazo zinapatikana kwenye iOS, Android na web huku ikiwa na jumla ya wasanii milioni 3.4 duniani kote.
Kwa kuanza na wasanii wa kiume watatu wa kwanza waliosikilizwa zaidi nchini Tanzania, Rayvanny anashika nafasi ya kwanza akifuatiwa na Diamond Platnumz katika nafasi ya pili huku Harmonize akishika nafasi ya tatu.

Wasanii wa kike watatu wa kwanza nchini Tanzania waliosikilizwa zaidi ni Zuchu akishika nafasi ya kwanza akifuatiwa na Nandy katika nafasi ya pili huku Maua Sama akishika nafasi ya tatu. Zuchu pia ametawala katika kipengele cha Nyimbo tatu kutoka kwa wasanii wa Tanzania zilizoongoza kusikilizwa ambazo ni Wana, Raha na Kwaru, zote hizo kutoka kwenye albamu ya Zuchu ‘I am Zuchu’.

Burna Boy ameongoza orodha ya wasanii wa kiume waliosikilizwa zaidi katika nchi zilizopo kusini mwa Jangwa la Sahara huku Simi akifanya hivyo kwa upande wa wasanii wa kike.
Boomplay pia imetoa taarifa za mwenendo na tabia za namna muziki unavyosikilizwa Tanzania. Katika taarifa hiyo maalumu, Bongo Flava imeongoza kwa kusikilizwa ikifuatiwa na nyimbo za Injili (Gospel) huku Afropop & Afrofusion ikishika namba tatu.

Zaidi, angalia hapo chini orodha kamili ya Boomplay 2020 Music Facts Tanzania. Msanii wako umpendaye, wimbo au albamu umeona? Tuambie!

Boomplay ni huduma ya kusikiliza na kupakua muziki kutoka Transsnet Music Limited. Kampuni hii ina ofisi nchini Tanzania pamoja na Kenya, Ghana na Nigeria. Mpaka kufikia Novemba 2020, watumiaji wa kila siku (DAU) ni milini 11 na kwa mwezi (MAU) watumiaji milioni 50. App hii pia inaendelea kuwa kinara katika apps za muziki barani Afrika.

Boomplay Music Facts Report Tanzania
Boomplay inatoa ripoti ya kila mwaka inayoonyesha trend za muziki, aina za muziki na wasanii waliosikilizwa zaidi kwa mwaka.

Vipengele vinajumuisha wasanii wa kiume na wa kike waliosikilizwa zaidi (Tanzania, Kusini mwa jangwa la Sahara na nje ya nchi), wasanii wapya, nyimbo zilizosikilizwa zaidi (Tanzania na nje ya nchi), albamu zilizosikilizwa zaidi (Tanzania na nje ya nchi pamoja na aina za muziki zilizosikilizwa zaidi.
18 Desemba 2020
Dar es Salaam, Tanzania

