Bunge la Venezuela latangaza tume ya kufuatilia suala la Rais Maduro

Waziri mmoja wa Venezuela ametoa taarifa ya kuundwa tume maalumu katika bunge la nchi hiyo ya kumkomboa Rais Nicolas Maduro kutoka kwenye makucha ya Rais Donald Trump na wenzake.
Kwa mujibu wa Russia Today, Waziri wa Mawasiliano wa Venezuela ametangaza kwamba tume hiyo imeundwa katika bunge la nchi hiyo ili kufuatilia mchakato wa kumkomboa Rais Nicolas Maduro. Ameongeza kwamba rais wa mpito wa Venezuela ameunda tume hiyo maalumu wakati wa mkutano wa baraza la mawaziri ili ifanye kazi ya kumkomboa Rais Maduro na mkewe.
Kutekwa nyara Rais Maduro na mkewe wakati wa uvamizi wa kijeshi wa Marekani nchini Venezuela kumesababisha wimbi kubwa la kulaaniwa jinai hiyo ya Marekani kote ulimwenguni.
Itakumbukwa kuwa, wawakilishi wa nchi wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wamelaani kitendo cha Washington cha kumteka nyara Rais wa Venezuela, Nicolas Maduro.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeitisha mkutano wa dharura kujadili uvamizi huo wa Marekani dhidi ya Venezuela na kutekwa nyara kwa Rais Maduro. Mabalozi wa Marekani na Venezuela walishambuliana kwa maneno makali katika kikao hicho, huku Ofisi ya Katibu Mkuu wa UN ikieleza wasiwasi wake kuhusu mustakabali wa nchi hiyo ya Latini Amerika.
Balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa, Vassily Nebenzia, amesema: Kutekwa nyara Rais wa Venezuela Nicolas Maduro na Marekani kunatishia kuirudisha dunia katika enzi ya “machafuko na dhuluma.”
Amesema Shambulio la Washington dhidi ya taifa la Amerika Kusini limeonyesha nidhamu ya dunia ambayo Marekani inataka kuiweka, mwanadiplomasia huyo alikiambia kikao cha dharura cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa jana Jumatatu.

