KAMATI ya Wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) leo inakutana jijini Dodoma kuridhia, Dk Tulia Ackson agombee uspika wa Bunge la Tanzania.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Rashid Shangazi alisema jana kuwa, kamati hiyo itakutana leo saa 8:00 mchana katika ukumbi wa Whitehouse mjini hapa.
Hivi karibuni, Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM ilipitisha jina la Dk Tulia awe mgombea wa kiti cha Spika kati ya majina 70 ya makada wa CCM waliochukua fomu na kurejesha kwa lengo la kuwania nafasi hiyo.
Utaratibu wa CCM ni kupeleka majina yasiyozidi matatu kwenye Kamati ya Wabunge kwa ajili ya kupigiwa kura na baadaye jina moja kuwasilishwa ofisi za Bunge.
Uchaguzi wa Spika utafanyika kutokana na nafasi hiyo kuachwa wazi na aliyekuwa Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai aliyejiuluzu Januari 6, mwaka huu.
Endapo Dk Tulia atapitishwa na Kamati ya Wabunge wa CCM na baadaye kuchanguliwa kwa kupigiwa kura wakati wa vikao vya Bunge zima kuwa Spika, itafanya kuwa mwanamke wa pili kuwa Spika baada ya Anne Makinda.