The House of Favourite Newspapers

CCM Wahofia Kuchukua Fomu za Uchaguzi Kibiti

1

 

Wakati hali ya wasiwasi ikizidi kushamiri kwa wakazi wa wilaya za Kibiti na Rufiji juu ya usalama wa maisha yao kutokana na kuendelea kwa matukio ya mauaji, hofu hiyo bado imetanda miongoni mwa wanachama wa CCM wanaohofia kuchukua fomu za kuwania uongozi ngazi ya matawi na shina.

 

Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu, Katibu wa Siasa na Uenezi wa chama hicho katika wilaya hizo, Mussa Mnyeresa amesema sababu za wanachama kususa kuchukua fomu hizo hasa ngazi za tawi, shina na  nafasi nyingine ni mfululizo wa matukio ya mauaji yanayoendelea katika wilaya hizi.

 

Amesema katika wilaya ya Kibiti, kata za Mjawa, Ruaruke na Mchukwi yanaongoza kwa wanachama wa chama hicho kutochukua fomu za kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.

 

Aidha amesema katika wilaya ya Rufiji uchukuaji fomu za nafasi za uongozi Tarafa ya Ikwiriri yenye Kata tatu za Umwe, Mgomba na Ikwiriri napo zoezi la uchukuaji fomu wa nafasi hizo si la kuridhisha.

 

Mnyeresa amesema hadi sasa kasi ya uchukuaji fomu hizo katika kata hizo bado ipo chini huku viongozi wa chama hicho wakiendelea kuwahamasisha wanachama wa chama hicho wachukue fomu.

 

Amesema uongozi wa chama hicho ngazi ya wilaya hizo ambazo awali ilikuwa ni wilaya moja tayari umepeleka taarifa za wanachama kwenye baadhi ya maeneo kutochukua fomu za kugombea nafasi mbalimbali wakihofia usalama wao.

 

Akizungumza juu ya wanachama kuchukua fomu za uongozi Ngazi ya Tawi na Shina katika wilaya ya Kibiti, Katibu wa chama hicho wilayani hapa, Zena Mgaya amesema hali ya uchukuaji fomu kwenye ngazi hizo hairidhishi.

 

Zena alisema katika ngazi za uongozi za kata na wilaya hali inaridhisha na wanachama wamehamasika kuchukua fomu hizo.

CREDIT: Mwananchi

1 Comment
  1. […] karibuni na mwanaharakati ambaye pia aliwahi kuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Sengerema kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) mwaka 2015, Laurence Mabawa, inatarajiwa kuanza karibuni. Akizungumza na wanahabari jijini Dar es […]

Leave A Reply