
DAKTARI bingwa wa upasuaji wa kurekebisha maumbile, Michael Obeng, Mmarekani mwenye asili ya Ghana, amefanikiwa kubandua gundi iliyokuwa imegandishwa kwenye ngozi ya kichwa cha mwanamke mmoja.
Mwanamke huyo alijipaka gundi hiyo bila kujua akidhani ni mafuta ya kurembesha nywele zake, kwa mujibu wa video za TMZ. Dkt. Obeng alichukua saa nne kuondoa gundi hiyo kutoka kwenye kichwa cha Tessica Brown, tovuti hiyo imeandika.
Daktari huyo bingwa aliyesomea chuo kikuu cha Havard, ambaye sasa hivi anaendesha shughuli zake katika eneo la Beverly Hills alijitolea kufanya upasuaji huo ambao ungegharimu dola 12,500 bila malipo baada ya kusikia masaibu yaliyompata Bi. Brown kupitia video ya TikTok wiki iliyopita.
Mwanamke huyo alikuwa ametumia gundi inayotumiwa kugandisha vigae, sakafu za mbao na mapambo ya nyumbani na kulazimika kukata nywele ambazo alikuwa amebandika kwa sababu zilikuwa zinavuta ngozi yake kwa nguvu.
Baada ya kupata matibabu, Brown aliyejawa na hisia kali, alionekana akipitisha vidole vyake kwenye nywele zake. Dkt. Obeng, ambaye ana historia ya utaalamu wa kemia, ameilezea TMZ kwamba alitumia kemikali mbalimbali kulainisha kiungo cha msingi (polyurethane,) kwenye gundi hiyo aina ya Gorilla Glue.

Alisema alifanya utafiti huo na kufanikiwa kutengeneza mchanganyiko wa kemikali kuondoa gundi hiyo iliyojumuisha aloe vera, mafuta ya mzaituni na nyinginezo. Baada ya kumaliza kutengeneza mchanganyiko huo, kwanza alijaribu katika nywele zilizokuwa zimegandishwa kwa aina hiyo ya gundi ili kuhakikisha kwamba itafanya kazi.
“Ana bahati kwa sababu hakupata majeraha makubwa katika ngozi yake ya kichwa. Aina hii ya gundi huwa sio mchezo,” alisema, na kuongeza kuwa gundi hiyo ilifanya nywele zake kugandia kama kijiti.
Alitoa wito kwa watu kuwa makini zaidi na kusoma vichupa vya kemikali mbalimbali wanavyonunua kabla ya kuanza kutumia bidhaa hizo.
Obeng amebobea katika upasuaji wa kubadilisha maumbile na kulingana na tovuti hiyo, yeye ni mwanzilishi wa shirika ambalo hufanya upasuaji wa bure katika mataifa yanayoendelea kukua na pia hutoa mafunzo kwa madaktari wa maeneo husika.
Chanzo- BBC SWAHILI

