Video: Dkt. Bashiru: Samia Atashinda Uchaguzi wa 2025 kwa Kishindo

Mratibu wa Kampeni za Kitaifa za Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Katibu Mkuu mstaafu wa chama hicho, Dkt. Bashiru Ali, amesema ana uhakika kuwa Mgombea Urais wa CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ataibuka na ushindi wa kishindo katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Akizungumza Jumatano, Septemba 10, 2025, katika mkutano uliofanyika Nzega Mjini, Tabora, Dkt. Bashiru amesema mwitikio mkubwa wa vijana na wanawake wanaojitokeza kwenye kampeni za CCM ni ishara tosha ya ushindi mkubwa unaosubiriwa.
“Tumekuwa na kiwango cha chini sana cha wapigakura kwa muda mrefu, siyo mwaka huu pekee wala 2020, lakini sasa nina uhakika kutokana na hamasa ya akinamama na vijana, tunaweza kufikia zaidi ya asilimia 90 ya wapigakura mwaka huu. Vijana ndiyo wengi, akinamama ndiyo wengi katika nchi hii,” amesema Dkt. Bashiru.
Ameongeza kuwa serikali ya CCM itaendelea kuhakikisha usalama wa kila aliyejiandikisha ili wananchi wapige kura kwa amani na kusherehekea ushindi bila hofu.
Kwa mujibu wake, katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Dkt. Samia, jumuiya za chama zimeimarika kwa kiwango kikubwa ikilinganishwa na kipindi cha nyuma, jambo alilolieleza kuwa limeongeza mvuto wa chama na mgombea wake.
“Mwitikio na mafanikio makubwa yaliyopatikana kwenye utekelezaji wa shughuli za maendeleo, pamoja na mvuto wa mgombea wetu, unatupa uhakika wa kushinda kwa kura nyingi,” amesisitiza.
Aidha, Dkt. Bashiru amesema kampeni za kisiasa ni fursa muhimu ya wananchi kueleza hisia zao kuhusu maisha, uendeshaji wa nchi na matarajio yao ya baadaye, akibainisha kuwa Tanzania imejengeka katika misingi imara ya amani na mshikamano. “Kampeni ni fursa ya kuwajengea wananchi matumaini na matarajio.
Kwa nchi ambazo hazina misingi imara, kampeni huwa chanzo cha vurugu na migawanyiko, lakini kwa Tanzania nafasi hiyo haipo. Hata hivyo, tusibweteke,” ameonya.