The House of Favourite Newspapers
gunners X

Dkt. Mwigulu Awataka Wakuu wa Mikoa Kuimarisha Utekelezaji wa Majukumu Nchini

0
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, Novemba 27, 2025 ameongoza kikao kazi maalum kilichowakutanisha Wakuu wa Mikoa wa Tanzania Bara, kikao kilichofanyika katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Mlimwa jijini Dodoma.

Kikao hicho kimeitishwa kwa lengo la kupitia mwenendo wa utendaji wa Serikali katika ngazi za mikoa, kuimarisha uratibu wa shughuli za kiserikali, pamoja na kujadili changamoto na mafanikio ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika maeneo mbalimbali nchini.

Akifungua kikao hicho, Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu amewasisitiza Wakuu wa Mikoa kuhakikisha kuwa serikali inabaki karibu na wananchi kwa kutatua changamoto zao kwa wakati, kusimamia kwa weledi miradi ya kimkakati, na kuhakikisha nidhamu ya utendaji inazingatiwa katika ngazi zote.

“Tunahitaji kasi mpya, uwajibikaji, na usimamizi thabiti wa fedha za umma. Hii ni Serikali ya matokeo, na lazima tuhakikishe kila mradi unaonekana na unawanufaisha wananchi,” alisema Dkt. Mwigulu.

Aidha, Waziri Mkuu amewataka viongozi hao wa mikoa kuimarisha ulinzi na usalama, kuendelea kushirikiana na vyombo vya dola katika kudhibiti vitendo vya uhalifu, pamoja na kuimarisha mazingira ya uwekezaji na biashara katika mikoa yao.

Kwa upande wao, baadhi ya Wakuu wa Mikoa walitoa taarifa fupi kuhusu mambo yanayoendelea katika maeneo yao, zikiwemo hatua za ukamilishaji wa miradi ya miundombinu, elimu, afya, kilimo na uwekezaji.

Kikao hicho kinatarajiwa kuendelea kwa majadiliano ya kina juu ya masuala ya kiuchumi, mipango ya Serikali ya muda mfupi na mrefu, pamoja na kupokea maelekezo ya kitaifa yatakayosaidia kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya mikoa.

 

Leave A Reply