Dkt. Samia Awaeleza Wananchi Jinsi ya Kupiga Kura Oktoba 29

Mgombea wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameendelea na mikutano yake ya kampeni mkoani Mwanza, ambapo leo Oktoba 7, 2025, amefanya mkutano mkubwa wa hadhara na kuwasihi wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki uchaguzi mkuu Oktoba 29.
Katika mkutano huo uliofanyika jijini Mwanza, Dkt. Samia aliwaonesha wananchi mfano wa karatasi ya kupigia kura, akielezea kwa undani namna ya kutambua alama ya CCM na sehemu sahihi ya kupiga kura.

“Ifikapo Oktoba 29, kwenye karatasi ya kupigia kura, juu kabisa utaona jina la Chama Cha Mapinduzi (CCM) upande wa kushoto, na jina la Mgombea Urais pamoja na Mgombea Mwenza yakiwa sambamba na picha zetu. Ukifika hapo, weka alama ya ✅ upande wa kulia — hapo utakuwa umeipa CCM ridhaa ya kuendelea kuongoza nchi yetu ya Tanzania,” alisema Dkt. Samia.
Akiwaomba wananchi kuendelea kuamini sera na dhamira ya CCM, Dkt. Samia alisisitiza kuwa serikali yake itaendeleza kasi ya maendeleo katika sekta za elimu, afya, maji, nishati na miundombinu, ili kuhakikisha Watanzania wote wanapata huduma bora na zenye usawa.
“Usikubali kupoteza haki yako. Shiriki uchaguzi, na mchague SAMIA kwa mitano tena, kwa maendeleo ya kweli ya Watanzania wote,” alisisitiza.
