The House of Favourite Newspapers

FAIZA ALLY: ALIPAMBANA USIKU NA MCHANA KUSAKA MAISHA BORA

 

 

Msanii wa Bongo movie Faiza Ally.

FAIZA Ally ni mmoja wa waigizaji wa sinema za Kibongo ambao kwa hivi sasa wameweza kujipatia umaarufu mkubwa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii na hata kwenye jamii.

 

Wengi walikuwa wakimfahamu kutokana na vituko mbalimbali alivyokuwa akifanya ambapo wengi wao walikuwa hawamuelewi na kumchukulia tofauti kabisa. Wapo waliomuona kama namna gani vipi! Faiza ni mzazi mwenza wa Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’.

Ni mmoja wa wanawake mastaa ambao wamepitia msoto mkali sana hadi kufikia hapo alipo. Kwa sasa anawatunza peke yake watoto wake wawili.

ALITOKEA WAPI?

“Mimi nilizaliwa mkoani Dodoma (kwa sasa ni jiji) nikiwa mtoto wa mwisho katika familia yetu. “Nilipitia maisha ya shida sana, japokuwa baba yangu alikuwa na uwezo mkubwa sana, lakini sikutaka kuwa tegemezi.
“Kwa kuwa nilikuwa sipendi kitu kinachoitwa umaskini hata kidogo, niliamua kuondoka nyumbani kwa wazazi wangu nikiwa na umri mdogo ili tu niweze kuwasaidia ndugu zangu kwani nilichukia sana umaskini tangu zamani.

 

AANZA KUFANYA KAZI KUSAIDIA NDUGU ZAKE!

 

“Unajua niliamua kuondoka
nyumbani ili tu nione kama naweza kuwasaidia ndugu zangu, lakini Mungu najua alisimama na mimi kwa sababu nilikuwa na nia hiyo tangu zamani hivyo nilianza kufanya kazi za hapa na pale na nyingine nakumbuka ilikuwa kampuni ya kuuza magari mimi nikiwa kama modo wao.

Hapo FAIZA nilianza kupata hela ambayo ilikuwa nikiwasaidia ndugu zangu niliowaacha Dodoma, ambao wengine wameshamaliza mpaka kidato cha nne.

 

AKUTANA NA SUGU “Katika harakati zangu za hapa na pale ndipo mwaka 2011, nilipokutana na Sugu kwenye Mtandao wa Facebook,
aliponitongoza sikujua kabisa kama ni mbunge na tulipokubaliana kisha tulikutana na mwisho tukaanza kuishi pamoja mpaka tulipozaa mtoto Sasha, lakini kukatokea kitu kidogo tu, tukatengana japokuwa nilikuwa nikijishusha mara nyingi
sana ili tumalize tofauti zetu tulee watoto wetu.

AANZA KUSOTA NA MAISHA

 

“Nikiwa tayari nimeshatengana na baba Sasha, nilikuwa kwenye hali mbaya sana na maumivu makali ukizingatia huku nina mtoto mdogo hivyo nilijikaza na kuona kuwa mimi ndiye mwenyewe ninaweza kusimama au kujikatili maisha yangu. “ilibidi niinuke na kuanza kufikiria kitu cha kufanya ambapo nilianza kufungua duka la nguo za kuogelea za watoto. Kwa kweli zilinisogeza sana na hapohapo nikapata wazo la kuanza kuuza nywele kwenye mitando na hilo pia lilinipeleka sehemu nyingine ya kuweza kuwaagizia watu mbalimbali kutoka China mpaka hapa.

 

AANZA KUYAFURAHI MAISHA YAKE

“Baada ya kuanza kufanya biashara ya kuwachukulia watu bidhaa mbalimbali kutoka China, nimejiona ni mwanamke ambaye nimeweza kusimama mwenyewe kama mama au kama baba, lakini kutokana na maisha ya taabu niliyopitia yamenifunza mengi sana na kunifanya leo niwe shujaa na bado sijafika kwani nataka niwe mwanamke tajiri.”

MAKALA NA IMELDA MTEMA | IJUMAA

Comments are closed.