The House of Favourite Newspapers

HADITHI YA KUSISIMUA: THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 10

0

MTUNZI: Hashim Aziz (Hashpower)

0719401968

ILIPOISHIA:

Licha ya kukimbia kwa kadiri ya uwezo wangu, yule konda bado alikuwa akija kwa kasi ya kimbunga, nikashtukia akinikata mtama wa nguvu kutokea nyuma, nikaruka na kudondoka chini kama mzigo, ile najaribu kunyanyuka tena alinifumua teke jingine kwa nguvu, nikaanguka tena, akaja na kunikalia kifuani.

 

“Muache inatosha jamaa! Oyaa anaua huku,” nilisikia mtu akipiga kelele lakini konda hakutaka kuniachia, alianza kunivurumishia ngumi za usoni, nikajua nisipofanya kitu kweli anaweza kuniua.

 

SASA ENDELEA…

Sijui kwa nini watu wengine wanakuwa na roho mbaya kiasi hiki, yaani amenikata mtama, nimedondoka na kuumia, ameona haitoshi, amenipiga tena teke na kuja kunikalia na kuanza kunitwanga ngumi za usoni kama anapigana na mtu mzima mwenzake.

 

Aliponipiga ngumi ya kwanza, niliona kama nyotanyota, akanipiga nyingine, nikaanza kuhisi vitu vikichuruzika kwa wingi puani na mdomoni, akawa anataka kunipiga ngumi nyingine, nikapata akili ya haraka.

 

Niliudaka mkono wake mzito na kumpindua kwa staili ya kuunyonga mkono kama nataka kuuvunja, akadondoka chini mzimamzima. Kufumba na kufumbua, niliokota jiwe lingine kubwa lililokuwa pembeni ya pale nilipoangukia, nikalinyanyua kwa jazba huku nikipiga kelele.

 

Nililishusha kwa nguvu zangu zote na kama asingepata akili ya kukwepa, huenda huo ndiyo ungekuwa mwisho wake. Kitendo kile kilimshangaza kila mtu kwa sababu kilitokea kwa kasi kubwa mno.

 

Kwanza nadhani hata yeye mwenyewe aliogopa kwa jinsi nilivyounyonga mkono wake na kumuangusha wakati yeye ndiye aliyekuwa amenikalia kifuani.

 

Kitendo cha kumkosakosa na lile jiwe, kilizidi kumpa woga, akajua kweli naweza kuyakatisha maisha yake.

 

Akiwa bado amepigwa na butwaa, nililiokota tena lile jiwe, huwezi kuamini aliponiona nikijitayarisha kulivurumisha tena, alikurupuka na kuanza kukimbia, na mimi sikutaka kumuacha, nikawa namkimbiza huku nikitafuta upenyo wa kumtwanga nalo. Kibao kikawa kimegeuka.

 

Maumivu niliyokuwa nayahisi baada ya kunipiga ngumi za uso, yalinifanya niwe kama mwendawazimu, sikujali kwamba alikuwa mkubwa kuliko mimi, nilitaka na mimi nimshikishe adabu.

 

Nilipomkaribia, nililivurumisha tena kwa kasi kubwa, akawahi kulikwepa, likaenda kupiga nguzo ya umeme, watu wakawa wanapiga kelele kwa nguvu.

 

Sikukubali, niliokota lingine lakini wakati nainuka, nilishtukia mtu akinikamata kwa nyuma, nikageuka na kutaka kummalizia hasira zangu, kufumba na kufumbua nikajikuta nimekamatwa na zaidi ya watu wanne, wote wakinisihi niachane naye kwani naweza kupata kesi ya kuua.

 

Yule konda alikimbia mpaka kwenye gari, akapiga bodi kwa nguvu akimuamrisha dereva wake kuondoa gari, kweli akaliondoa kwa kasi huku watu wakicheka na wengine wakishangilia.

 

“Mngemuacha amkomeshe, hawa makonda wamezoea sana kuonea abiria,” alisema mtu mmoja huku wengine wakiendelea kunisihi nitulie.

 

Kwa jinsi nilivyokuwa na hasira, hasa baada ya kumuona amefanikiwa kuondoka na kukimbia, zilinifanya niwe nalia kwa jazba kama mtu aliyepandisha mashetani.

 

“Punguza hasira mdogo wangu,” alisema yule mwanaume aliyekuwa amenikamata mikono kwa nguvu akiendelea kunisihi.

 

Haikuwa kazi nyepesi kunituliza kwani hakuna kitu ambacho nilikuwa siwezi kukubaliana nacho kama kuonewa.

 

Basi wasamaria wema walifanikiwa kunitoa eneo hilo, wakanipeleka kwenye duka moja la dawa ambalo pia walikuwa wakitoa huduma za vipimo na kuchoma sindano.

 

Nikaingizwa ndani ambapo harakaharaka nilisafishwa damu zilizokuwa zinaendelea kunitoka, nikapewa dawa za kupunguza maumivu na angalau sasa nikawa najisikia vizuri.

 

“Kwani unaelekea wapi?” mmoja kati ya wale watu walionipeleka pale kupata huduma ya kwanza aliniuliza.

 

“Nimekuja town kutafuta maisha,” nilijibu bila hata kumtazama usoni, nikawa naendelea kujichua pale usoni kwa kipande cha barafu nilichopewa ambacho nilielezwa kwamba kitasaidia kukata damu zisiendelee kutoka puani.

 

“Una ujuzi gani kichwani?”

 

“Mbona unaniuliza maswali mengi,” nilisema huku nikimgeukia. Bado nilikuwa na hasira na nilimuona kama kila mtu ni mbaya kutokana na kilichotokea.

 

“Nguo yako imelowa damu, hebu nisubiri nikuchukulie hata jezi hapo nje! Usitoke, kaa hapahapa,” alisema huku akiinuka.

 

Alitoka na aliporudi, alikuwa na jezi ya Simba mkononi ambayo ilionesha ameinunua hapo nje, akanirushia na kuniambia nibadilishe na kuivaa.

 

Nilimshukuru, nikavua lile shati nililotoka nalo nyumbani ambalo kweli lilikuwa limelowa damu, nikajifutafuta vizuri na kuivaa ile jezi, akaniambia lile shati chafu nilitupe kwenye ‘dust bin’, jambo ambalo nililifanya.

 

“Lengo langu ni zuri tu mdogo wangu! Nimefurahishwa na ujasiri ulioonesha wa kukabiliana na yule mshenzi na ndiyo maana nipo hapa kukusaidia,” alisema mwanaume huyo. Nikamtazama vizuri usoni.

 

Alikuwa ni mtu wa makamo, akiwa amevalia koti la suti, ndani akiwa na fulana na shingoni akiwa na cheni kadhaa zinazong’ara na chini akiwa amevaa raba.

 

Alionesha kuwa mtu ambaye anajimudu kidogo kimaisha, nikashusha pumzi ndefu na kuendelea kumtazama mwili wake uliokuwa umejazia, akionesha wazi kwamba ni mtu wa mazoezi.

 

“Unaonaje tukawa na mazungumzo kidogo baada ya kutoka hapa? Usiwe na wasiwasi, mimi nitakulinda.”

 

“Sihitaji kulindwa, naweza kujilinda mwenyewe.”

 

“Hizo hasira umerithi kwa nani?” aliniuliza huku akichekacheka, sikumjibu chochote zaidi ya kujiinamia huku nikiendelea kuugulia maumivu ambayo sasa yalikuwa yamepungua sana.

 

Hata sijui nani alilipia ile huduma niliyoipata pale lakini baadaye, yule mwanaume ambaye bado sikuwa namjua ni nani na kwa nini ameamua kunisaidia, aliniambia tuondoke, nikainuka na kumfuata.

 

Nilichokigundua, kumbe hakuwa peke yake, alikuwa na wenzake kama watatu hivi ambao hata pale eneo la tukio niliwaona.

 

Wenzake walikuwa wamekaa upande wa mbele wa lile duka na ilivyoonesha ni kama hawakuwa wanataka watu wajue kama wapo pamoja maana hata sisi tulipotoka, nao waliinuka mmoja baada ya mwingine na wakawa wanakuja nyuma yetu.

 

“Hawa ni akina nani?” nilimuuliza yule mwanaume.

 

“Wako wapi?”

“Hao wanaokuja nyuma yetu?” nilimuuliza swali ambalo lilimfanya anitazame usoni na kutabasamu.

 

Umegunduaje kama wanatufuata?” alinijibu huku akitabasamu.

 

Basi kule nje watu bado walikuwa wamekusanyika kwa makundi makundi na waliponiona nimetoka, wengine walianza kupiga miluzi huku wengine wakishangilia.

 

“Umeshakuwa staa!” alisema yule mwanaume huku akinigeukia, nikashindwa kuelewa anamaanisha nini.

 

Mbele kidogo, tuliingia kwenye gari dogo lenye vioo vya giza (tinted), akanielekeza kukaa siti ya pembeni ya dereva wakati yeye akikaa nyuma ya usukani.

 

Muda mfupi baadaye, wale wanaume wengine ambao nilishawahisi kama wanatufuata kwa nyuma, nao waliingia na japokuwa gari lilikuwa dogo na wao kila mmoja alikuwa na mwili mkubwa, waliweza kutosha kukaa wanne kule nyuma.

 

“Dogo anataka kuwajua nyie ni akina nani?”

 

“Aah tusamehe mzee, usije kutuchenjia kama ulivyomchenjia konda,” alisema mmoja, wote wakacheka sana na wakawa wananisalimu kwa kunipa mikono ningongesheane nao, watoto wa mjini wanaipa kupeana tano.

 

“Usiwe na wasiwasi, hawa ni marafiki zangu na upo kwenye mikono salama,” alisema yule dereva huku akiondoa gari. Akaniuliza tena kama ni kweli nataka kazi.”

 

“Ndiyo nataka kazi braza,” nilimwambia, safari hii kwa upole na nidhamu kwa sababu nilishaona kweli ana nia ya kunisaidia.

 

“Tutakupeleka kwa bosi wetu, naamini huwezi kukosa kazi ya kufanya, hasa tukimsimulia ulivyotaka kumwaga ubongo wa konda wa daladala,” alisema, wenzake wote wakacheka sana na kugongesheana mikono.

 

Moyoni nilikuwa na hofu lakini sikutaka sana kuitanguliza hofu yangu maana ni kweli nilikuwa natafuta kazi na kilichotokea ilikuwa ni kama zari.

 

Basi tuliingia kwenye barabara ya lami na safari ya kuelekea mjini ikaendelea, wakawa wanapiga stori za hapa na pale na kucheka kwa nguvu.

 

Basi tulienda mpaka mbele kidogo, kwenye kituo kilichochangamka sana ambacho baadaye nilikuja kugundua kwamba panaitwa Mombasa. Kwa wenyeji wa Gongo la Mboto watakuwa wanapajua vizuri.

 

Basi dereva akapunguza mwendo na kutoka kwenye barabara ya lami, akaingia mpaka kwenye maegesho ya baa moja iliyokuwa jirani na barabara.

 

“Shuka mdogo wangu tukainue mioyo yetu,” alisema yule dereva huku akinipigapiga begani, watu wote wakashuka na mimi nikashuka, ‘aka-lock’ milango yote kisha wakatangulia na kuanza kupandisha kwenye ngazi za kuingia kwenye hiyo baada, na mimi nikawa nawafuata.

 

Tulipoingia kwenye baa hiyo, waliongoza moja kwa moja mpaka kwenye chumba kilichokuwa kimejitenga, ndani kabisa ambapo mlangoni kilikuwa na maandishi yaliyosomeka VIP.

 

Wakati tunapita, karibu watu wote waliokuwa ndani ya baa ile, waliacha kila walichokuwa wanafanya na kuanza kututazama.

 

Sikuelewa haraka kwa nini hali hiyo imetokea lakini sikutaka kuwa na haraka ya kujua mambo. Basi tuliingia mpaka kule ndani, wakaja wahudumu wa tatu wa kike waliokuwa wamevalia kihasarahasara, wakawa wanasalimiana nao kwa kukumbatiana na kupeana mabusu.

 

Ilionesha ni kama wanafahamiana kwa jinsi walivyokuwa wanachangamkiana. Muda mfupi baadaye, meza ilikuwa imejaa vinywaji, kuanzia pombe kali, bia za kawaida na pakti mbili za sigara.

 

Kwa fujo hizo ilionesha kwamba walikuwa na fedha za kutosha, nikawa nashangaashangaa tu.

 

Je, nini kitafuatia? Usikose kesho hapahapa! Unaweza pia kusoma au kusikiliza hadithi nyingine kwa kuingia:

www.simulizizamajonzi7113.blogspot.com , Facebook: Simulizi za Majonzi au Youtube:

 

Hashpower Online.

 

Usisahau kulike, share na ku-subscribe.

 

 

 

 

 

 

Leave A Reply