The House of Favourite Newspapers

HADITHI YA KUSISIMUA: THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 17

0


MTUNZI: Hashim Aziz (Hashpower)
0719401968
ILIPOISHIA:

Nilipofika tu getini, kabla hata sijagonga, mlango mdogo wa pembeni ulifunguka, mlinzi mwenye silaha, aliyevalia sare maalum alinikaribisha kwa kunionesha tu ishara kwamba niingie, nilipoingia geti lilijifunga, nikashusha pumzi ndefu wakati nikitembea harakaharaka kuelekea kule ndani.

SASA ENDELEA…
Kwa jinsi jengo hili lilivyojengwa, unapoingia tu unaweza kudhani kwamba ni karakana au gereji kubwa na ukiingia unawaona kabisa mafundi waliovaia sare maalum wakiwa bize na kazi zao, nadhani bosi Mute alifanya hivi kwa makusudi kabisa ili kuwapoteza ‘maboya’ watu wanaomfuatilia.

Kwa ndani kulikuwa na geti jingine na huko ndiko mambo yote yalikokuwa yakifanyika. Basi nilipoingia kwenye geti la pili tu, kila mtu aliacha alichokuwa anakifanya, wote wakawa wananitazama.

Kwa mbali nilimuona Bonta akifanya mazoezi ya kunyanyua vitu vizito na wenzake, akanipa ishara kwamba nimfuate pale alipo. Basi niliwapita watu wote bila kumsemesha mtu yeyote, nikaenda mpaka pale Bonta alipokuwa. Nilipomkaribia tu, simu yake ilianza kuita, akaitoa na kuipokea, nikamsikia akisema neno moja tu, ‘sawa’.

“Bosi anakuita, nifuate,” aliniambia, nikagundua kwamba lazima ile simu imetoka kwa Bosi Mute. Tukawa tunatembea kuelekea kulekwenye geti la tatu, ambako kuna ulinzi mkali zaidi.

“Umefikia wapi?”
“Nimekamilisha.”
“Umempeleka wapi?”
“Kariakoo.”
“Umeamuacha kwenye mazingira gani?”

“Kuna mama mmoja muuzaji wa duka la vipodozi ndiyo nimeamuachia.”
“Ulitumia mbinu gani?”

“Nilijifanya nataka kwenda chooni, akanipokea,” nilimwambia, akanitazama usoni kisha akaachia tabasamu, akanipigapiga begani na kuniambia: “Safi sana, naamini bosi atafurahi sana.”

Tuliingia kule ndani, kama kawaida tukakaguliwa na vifaa maalum, tukaingia sehemu ya pili kwenye jengo lenye vioo vitupu, milango ikafunguka yenyewe na kuingia mpaka ndani. Tulienda moja kwa moja mpaka kwenye ofisi ya Bosi Mute.

Tulipoingia tu, alisimama pale alipokuwa amekaa akichezea laptop yake, akatusogelea ambapo Bonta aliinama kutoa heshima, na mimi nikafanya hivyo.

“Nipe ripoti,” alisema, nikashusha pumzi ndefu na kumueleza kama nilivyomueleza Bonta, akafurahi sana ambapo kwa mara ya kwanza nililiona tabasamu kwenye uso wake.

“Karibu sana kwenye himaya yangu, kuanzia sasa utakuwa mwanachama kamili,” alisema huku akinipa mkono, akaniambia taratibu zote za kazi nitapewa na Bonta na kama kuna chochite nahitaji kujua kutoka kwake, milango iko wazi.

Alisogea kwenye kabati la ukutani, akafungua na kutoa burungutu la fedha, akampa Bonta na kumueleza maneno fulani kwa sauti ya chini ambayo mimi sikuyasikia, Bonta akawa anatingisha tu kichwa kuonesha kumuelewa.
“Kwa sasa nakuruhusu ukapumzike, maelezo yote nimempa kiongozi wako hapa,” aliniambia huku akitoa burungutu jingine la fedha na kunikabidhi, nikamshukuru sana huku moyoni nikiwa na furaha kubwa.

“Bosi anasema nikakutafutie chumba kizuri cha kupanga na kununua vitu vyote muhimu unavyotakiwa kuwa navyo ili kuanza maisha ya kujitegemea,” aliniambia Bonta wakati tukiwa tunatoka.

Suruali niliyovaa ilianza kunibana kwani upande wa kushoto kulikuwa na burungutu la fedha alizonipa mwanzo naupande wa pili kulikuwa na burungutu jingine alilonipa muda huo. Moyo wangu ulikuwa na furaha kubwa sana, nikawa najiambia ‘maisha si ndiyo haya!’.

“Bro, naomba na leo twende nyumbani nikapeleke hela za matibabu ya baba,” nilimwambia Bonta wakati akiwasha pikipiki lake kubwa, akiwa amenipakiza.

“Tufanye kwanza tulichoambiwa na bosi, usijali nitakupeleka,” alisema Bonta, nikafurahi sana ndani ya moyo wangu. Kiukweli hakuna kitu nilichokuwa natamani kukifanya kwa kadiri ya uwezo wangu wote kama kuwasaidia nyumbani.

Hali aliyokuwa nayo baba ilikuwa mbaya sana na mpaka muda huo, mimi ndiye niliyekuwa tegemeo. Japokuwa nilijua kabisa kwamba nimeingia sehemu mbaya, lakini kwa kuwa lengo langu la kuisaidia familia lilikuwa limeanza kutimia, niliamua liwalo na liwe.

Bonta alivuta mafuta kwa nguvu, pikipiki likapiga kelele kwa sauti ya juu na kutoa moshi mwingi, nikawasikia wale wafanyakazi wengine wakipiga miluzi kumshangilia Bonta, akaiondoa kwa kasi kubwa.

Tulitoka getini kwa mikwara ya hali ya juu, Bonta akivuta mafuta kwa nguvu na kufanya mlio wa pikipiki uwe kama wa helikopta mbovu, tukaingia barabarani na safari ikaendelea. Sikuwa najua tunaelekea wapi lakini nilichokuwa najua ni kwamba Bonta anaenda kunisaidia kutafuta sehemu ya kuishi.

Breki ya kwanza ilikuwa ni nyumbani kwa Bonta, Kipawa ambapo alipaki pikipiki, tukashuka na kuingia ndani. Tulipumzika kidogo kisha akaniuliza ningependa kuishi sehemu gani ambayo nitakuwa huru?
Ilibidi tu nimweleze ukweli kwamba Dar mimi ni mgeni, kwa hiyo yeye aangalie sehemu inayoweza kuwa nzuri kwangu.

“Unaonaje ukienda kuishi Sinza? Unajua hapa sheria yetu ni moja kwamba lazima kila sehemu awepo mtu anayeishi, lengo ni kusambaa jiji lote, usione mimi nakaa huku Kipawa, pale kuna watu wanaishi Makumbusho, Mwenge, Tegeta, Tabata, Vingunguti na sehemu nyingine kibao, wala huwa hatukai karibukaribu, hiyo ndiyo falsafa ya bosi,” alisema Bonta, nikawa namsikiliza kwa makini.

Niliunga mkono suala la kwenda kuishi Sinza kwa sababu nimekuwa nikisikia sana sifa za Sinza na kiukweli japokuwa nilikuwa siijui vizuri, sifa zake zilinifanya nitamani kwenda kuishi huko.

Baada ya kukubaliana, Bonta alichukua simu yake na kutafuta namba fulani kisha akaiweka simu sikioni. Kumbe alikuwa amempigia dalali wa vyumba, akamueleza kwamba anataka chumba kizuri Sinza, chenye hadhi nzuri.
“Kwa hiyo jioni saa ngapi?” nilimsikia akimuuliza, kisha akakata simu.

“Vyumba vipo, amesema twende saa kumi jioni,” alisema Bonta, nikashusha pumzi ndefu na kuchekelea ndani ya moyo wangu.

“Na mimi naenda kuwa na kwangu, mbona kama miujiza,” nilijisemea ndani ya moyo wangu huku nikitabasamu. Kiukweli sikuwahi kuishi peke yangu, maisha yangu yote yalikuwa ni nyumbani na sikuwahi kuishi nje ya himaya ya baba na mama.

Hakukuwa na muda wa kupoteza, baada ya kupumzika kidogo, tulitoka na Bonta mpaka Keko ambako aliniambia nichague ‘fenicha’ ninazozitaka. Safari hii tlitumia usafiri wa teksi, ile pikipiki yake akaifungia.

Aliniambia natakiwa kuishi maisha ya juu kama alivyokuwa akiishi yeye. Nilibaki nimepigwa na butwaa na nadhani aliligundua hilo, ikabidi yeye ndiyo awe mstari wa mbele kunichagulia kile alichoona kinanifaa.

Tulianza kwenye vitanda, akachagua kitanda kimoja kikubwa, kilichotengenezwa kwa mtindo wa kisasa, akaniuliza kama nimekipenda, nikajibu kwa kutingisha tu kichwa. Unajua kuna wakati furaha ikinizidi, huwa nashindwa kuongea, nakuwa kama nimebanwa na donge kubwa kooni, kama inavyotokea nikiwa na hasira na njia pekee inayoweza kunisaidia, ni kutoa machozi.

Nilitokwa na machozi ya furaha, Bonta akanitazama na kupigwa na butwaa, ilibidi anivute pembeni na kuniuliza nilikuwa na tatizo gani? Ilibidi tu nimweleze ukweli kwamba siamini kinachofanyika, akacheka sana na kunipigapiga mgongoni, akaniambia ‘yajayo yanafurahisha’.

Nilifuta machozi na kurudi kwenye hali yangu ya kawaida, tuliendelea na shopping ya nguvu, tulinunua pia set ya masofa ya kisasa, kabati la nguo, dressing table na meza ya kulia chakula. Vitu vilikuwa vingi sana, nikawa najiuliza tutavibebaje?

Kumbe alishaweka mipango yake vizuri kwani wakati tunaendelea kuchagua, kuna mtu alimpigia simu, nikamsikia akimwambia kwamba apaki pembeni ya barabara. Baada ya kumaliza, akiwa ameshalipa kila kitu kwa kutumia zile fedha alizopewa na Bosi Mute, tulitoka mpaka barabarani, tukakuta kuna gari aina ya ‘Canter’ limepaki.

Akaenda kuzungumza na dereva, nikaona ameanza kulirudisha nyuma, akalipaki vizuri, vijana wa kubeba mizigo wakamsunguka Bonta ambapo alianza kutoa maagizo kibabe, vile vitu vyote tulivyonunua vikaanza kutolewa na kupelekwa kwenye ile Canter huku sisi tukiwa tumesimama pembeni tukihakikisha kila kitu kinaenda sawa.

Baada ya kumaliza, aliwalipa wale wabeba mizigo, sisi tukaingia ndani ya gari na safari ya kuelekea Sinza ikaanza. Mbele kidogo alimweleza dereva kusimamisha gari, tukashuka tena na kuingai kwenye duka kubwa la vifaa vya nyumbani, tukanunua godoro kubwa na vikorombwezo vingine, yakiwemo mapazia, meza ya vioo, mazulia na vifaa vingine.

Tukarudi kwenye gari na safari ikaendelea. Tulienda mpaka Sinza Madukani ambapo gari lilipaki pembeni, mimi na Bonta tukashuka kwenda kukutana na dalali. Alipotuona, alituchangamkia sana, tukaongozana naye mpaka kwenye nyumba aliyopata.

Unajua fedha zinaleta ujeuri sana! Hebu vuta picha, mnaenda kufanya manunuzi ya vifaa kibao vya ndani wakati hata chumba chenyewe hamjakiona! Ninavyojua mimi, watu wengi huwa wanaenda kwanza kukagua nyumba, kupatana na mwenye nyumba na wakikubaliana kiasi wanachoweza kukimudu cha kodim, ndiyo mambo mengine yanafuatia, lakini kwetu sisi ilikuwa kinyume.

Tulipelekwa mpaka kwenye nyumba moja nzuri, iliyokuwa na geti jeusi. Ilikuwa ni nyumba nzuri kwelikweli, nikisema hivyo naomba nieleweke! Kwanza ilikuwa ikijitegemea kwa kila kitu, kulikuwa na geti la peke yake, ndani kulikuwa na sehemu ya ‘parking’ ya magari, korido kubwa iliyopigwa marumaru safi kabisa.

Je, nini kitafuatia? Usikose kesho hapahapa! Unaweza pia kusoma au kusikiliza hadithi nyingine kwa kuingia:

www.simulizizamajonzi7113.blogspot.com , Facebook: Simulizi za Majonzi au Youtube: Hashpower Online.

Usisahau kulike, share na ku-subscribe.

Leave A Reply