The House of Favourite Newspapers

HADITHI YA KUSISIMUA: THE DARKEST HOURS(SAA ZA GIZA TOTORO)-27

0

Mtunzi: HASHIM Aziz (Hashpower)

0719401968

ILIPOISHIA:

Alikuwa akitaka kuniletea uongo wa waziwazi, bila shaka sote tunawafahamu wale watu wanaofanya kazi mapokezi au kwa kiingereza receptionist. Eti alitaka kuniaminisha kwamba yeye ni mtu wa mapokezi tu, wakati muda mfupi uliopita alinitolea bastola na kuniuliza kama najua kuitumia.

SASA ENDELEA…

Inawezekanaje mtu wa mapokezi akawa na bastola kiunoni?

“Anyway tuachane na hayo, mi naitwa Kezia, wengi wamezoea kuniita Lady Keys, nafurahi kufahamiana na wewe,” alisema huku akinipa mkono, na mimi nikanyoosha mkono wangu na kumpa.

 

Kwa mwonekano wake na jinsi alivyokuwa mrembo, ungetegemea kwamba mkono wake utakuwa ‘softi’, lakini niliposhikana naye, nilishtuka kidogo kugundua kwamba alikuwa na mkono mgumu kwelikweli, wakati nikimshangaa, akaniwahi.

 

“Una mkono mgumu sana, wewe ni mtu wa kazi eeh?”

“Na wewe una mkono mgumu sana receptionist,” nilimjibu, akaishia kucheka tu maana niliamua kuwa ‘kauzu’ sana kwake.

 

“Karibu ukae,” alisema, safari hii kwa nyodo za kikekike, ule ‘ugumu’ aliotaka kunionesha ulianza kupungua kadiri muda ulivyokuwa unasonga mbele. Bila hata kuniuliza, aliingia kule ndani na kwenda kufungua friji, akatoa chupa mbili za bia na kuja nazo pale akiwa ameshazifungua, moja akanipa huku akiendelea kuvuta sigara na kutoamoshi mwingi.

 

“Afadhali nimepata mshikaji wa kupiganaye stori, ujue hapa wamejaa watu wa ajabuajabu, hata sina wa kupiga naye stori, isitoshe wengi ni wakubwa na wakija hapa kazi yao ni kunitongoza na kunitishia tu,” alisema msichana huyo ambaye sasa nilikuwa nalijua jina lake, Kezia.

 

“Usijali, nimefurahi pia kukufahamu Kezia,” nilimwambia huku nikipiga funda moja na kumtazama, akatabasamu.

“Na wewe ulikuwa miongoni mwa walioshiriki tukio la Tandika,” aliniuliza, nikamjibu kwa kutingisha kichwa.

 

“Mh! Mbona nasikia machalii wote walipigwa ‘gani’ wakatoka wakongwe watupu?” aliniuliza, nikapiga funda jingine kisha nikamtazama tena.

 

“Mimi nilitoka salama,” nilimjibu huku nikijiinamia, nikacheua povu la bia na kukaa vizuri.

 

“Daah! Noma sana mshkaji wangu, nakaumbuka na mimi kwenye tukio langu la kwanza nilitoka peke yangu, wenzangu wote tulioingia nao walikula mashine palepale huku nikiwashuhudia, dah! Hizi kazi hizi,” alisema huku naye akipiga funda kubwa na kucheua.

 

Sasa nilishapata uhakika wa kile nilichokuwa nakihisi! Keshia alikuwa sawa na mimi, hakuwa mtu wa reception wala nini, alikuwa jambazi. Unajua tofauti na zamani ambapo tulikuwa tukiaminikwamba majambazi ni ‘mijitu’ flani hivi ya kutisha, siku hizi huwezi kumdhania mtu kama ni jambazi, mpaka labda akamatwe.

 

Kwa mwonekano wake, Kezia alikuwa bonge la sistaduu, mzuri wa sura na umbo na anajipenda kwelikweli maana pale pote tulipokaa palikuwa pakinukia pafyumu aliyojipulizia, usingeweza kuamini kama ni mtu wa kazi, kama ambavyo usingeweza kudhani kama na mimi nashika mashine.

 

“Ilikuwaje?” nilimuuliza kwa udadisi, akashusha pumzi ndefu na kutulia kwa sekunde kadhaa. Akaanza kuniambia kwamba yeye ni mzaliwa wa Musoma, alikuja Dar es Salaam kutafuta maisha lakini siku za mwanzo akawa hana mbele wala nyuma, akawa anaishi kwa kubangaizabangaiza mpaka siku alipokutana na wanawake wawili waliomuunganisha na Bosi Mute.

 

Aliniambia kwamba Bosi Mute alipokutana naye kwa mara ya kwanza, alionesha kuvutiwa naye sana, akajitolea kwenda kumsomesha kazi ya ureceptionist huku akimilipia kwa kila kitu, akampangia chumba na akawa anampa fedha za kutosha.

 

“Nilisoma kwa miezi mitatu tu, nikapata cheti na kupelekwa kwenye ofisi yake ya Kariakoo, nikawa nafanya kazi kama receptionist,” aliniambia na kunifungua kichwa kwamba kumbe Bosi Mute ana ofisi nyingine Kariakoo.

 

Alinisimulia vitu vingi vilivyoendelea mpaka mwisho alipojikuta akiingia kwenye kazi ya kushika mtutu wa bunduki.

 

“Kiukweli sikulazimishwa ila mazingira tu yenyewe yalinifanya nikose cha kufanya zaidi ya kukubali kujiunga na vijana wa Bosi Mute, tukapelekwa mafunzoni huko Kisarawe ambako nilifundishwa na wenzangu namna ya kutumia bunduki kisha wikikadhaa baadaye, ndiyo tukapangiwa kwenda kufanya tukio Kariakoo, kwenye ofisi za Wahindi fulani waliokuwa wakifanya kazi ya kubadilisha fedha za kigeni.

 

Alinieleza jinsi walivyovamia wakiwa kama kumi hivi, wakaisimamisha Kariakoo yote kwa dakika kadhaa na kufanikiwa kupora kiwango kikubwa cha fedha kabla ya baadaye polisi kuvamia na kusababisha iibuke vita kali ya kurushiana risasi.

 

“Wenzangu wanne ambao nilitoka nao mafunzoni walipigwa risasi palepale, wawili wasichana kama mimi na wengine wawili wavulana, yaani sitakuja kuisahau ile siku,” aliniambia huku akitikisa kichwa chake kwa masikitiko.

 

Stori yake ilikuwa ikifanana sana na ya kwangu, akaendelea kunieleza kwamba baada ya msako kuwa mkali, yeye na wenzake waliotoka salama wakahamishiwa Kibaha na kuanzia siku hiyo ndiyo alipoanza kuishi hapo kambini.

 

“Sasa hivi kukitokea kazi, tunatoka usiku na kwenda kupiga dili kisha tunarudi hapahapa! Nimeshakuwa mzoefu,” alisema kwa kujiamini. Maelezo yake yalinifanya nivutiwe naye na kumuamini sana, nikaona nimepata kampani ya nguvu.

 

“Kwa hiyo wewe unaishi hapahapa?”

“Siyo mimi tu, tupo kibao! Utawaona wengine muda ukifika!” aliniambia, tukaendelea kupiga stori za hapa na pale, nikamwambia kwamba jina langu naitwa Kenny au Snox na nikamueleza kwa kifupi kuhusu maisha yangu.

 

Sikumueleza mambo mengi kuhusu mimi, basi tukaendelea kupiga stori huku tukishushia na bia ambazo alikuwa akienda kuchukua na kuzifungua kwa sababu zilikuwepo za ‘kumwaga’.

 

Baadaye alienda kuleta chakula, tukala pamoja huku stori zikiendelea. Baadaye, alikuja mwanamke mmoja mtu mzima kiasi, akaniuliza kama mimi ndiyo Kenny, nikamkubalia, akaniambia nimfuate.

 

“Uje basi ukimaliza,” aliniambia Kezia huku akionesha kuanza kuchangamka kutokana na kilevi, nikamuonesha kwa ishara kwamba nitarudi. Yule mwanamke alinipeleka mpaka kwenye jengo la sita kutoka pale tulipokuwepo, kama nilivyoeleza kulikuwa na majengo mengi yaliyojengwa kwa mpangilio.

 

“Hapa ndipo utakapokuwa unaishi, hiki ndiyo chumba chako, kina kila kitu ndani na ukihitaji chochote, kuna simu ya mezani utanipigia,” alisema yule mwanamke ambaye baadaye alijitambulisha kwamba yeye ndiyo Matron.

 

“Nashukuru sana,” nilisema wakati nikipokea funguo, basi akaondoka zake na kuniacha naendelea kukagua kile chumba. Jengo zima lilijengwa kwa mfumo kama wa hosteli hivi, kulikuwa na vyumba vingi ambavyo vilikuwa vinajitegemea. Mle ndani mlikuwa na chumba cha kulala chenye kitanda kikubwa, meza ndogo, friji dogo, kabati la nguo na vyoo na bafu ndani kwa ndani.

 

Nilishusha pumzi ndefu na kujilaza kitandani, ni hapo ndipo nilipogundua kwamba kumbe nilikuwa nimeanza kulewa. Niliinuka na kwenda kufungua lile friji dogo, nikakuta ndani kuna maji na chupa kadhaa za pombe! Nikachukua bia moja na kuifungua, nikaendelea ‘kujimiminia’, sikutaka kukumbuka chochote kilichotokea Dar es Salaam.

 

Haukupita muda mrefu, nikapitiwa na usingizi mzito, nilikuja kuzinduka baada ya kusikia mlango ukigongwa, nilipotoka nilikutana na mzee wa makamo akiwa na sinia lililokuwa na chakula, tukasalimiana kisha akaniambia huo ni msosi wangu.

 

Sikushangaa sana kwa sababu kwa fedha tulizokuwa tukimuingizia Bosi Mute, alikuwa na haki ya kutuhudumia kama wafalme. Basi niliingia ndani na kuufakamia msosi wote, nikavitoa vyombo nje kama alivyonielekeza yule mzee kisha nikarudi na kwenda kujimwagia maji kupunguza uchovu.

 

Nilirudi na kujilaza kitandani nikiwa nimejifunga taulo, nikawa nachezea simu yangu, mara nikasikia kitasa cha mlango kikikandamizwa taratibu kuelekea chini, nikakaa makini kutaka kujua ni nani aliyekuwa akiingia. Nilishtuka kugundua kwamba ni Kezia, nikashusha pumzi ndefu na kujiweka vizuri pale kitandani.

 

Alikuwa amebadilisha nguo na kuvaa kigauni fulani chepesi kilicholifanya umbo lake zuri lionekane vizuri, akaufunga mlango kimyakimya na kumalizia kwa kufunga na funguo kabisa.

 

“Sitaki wajue kama nipo huku,” aliniambia kwa sauti ya chini huku akicheka, akaja mpaka pale kitandani, akajitupa na kunisogelea.

 

“Vipi mwanangu, mbona nimekwambia urudi halafu umenichunia,” alisema kwa Kiswahili cha kihuni, nikacheka kidogo na kumwambia kwamba nilikuwa najihisi kulewa, akacheka na kupeleka mkono wake kifuani kwangu.

 

“Yaani muda mfupi tu niliokaa na wewe nimejikuta nimekuzoea utafikiri tumejuana miaka kumi iliyopita,” aliniambia huku akijisogeza mwilini mwangu. Sikuweza kujizuia, na mimi nikapeleka mkono wangu kwenye kiuno chake na kumshika, akashtuka kidogo halafu akanitazama.

 

“Nimekuwa mpweke kwa siku zote ninazoishi kwenye hili gereza, leo nimefurahi sana umekuja,” aliniambia huku na yeye akiupitisha mkono wake taratibu kwenye kifua changu.

 

Kama nilivyosema, Kezia alikuwa sistaduu haswaa! Chumba chote kilikuwa kimejawa na harufu ya marashi mazuri aliyojipulizia. Alikuwa mzuri sana kwa sura na umbo, ukizingatia tayari na mimi nilishaujua utamu wa mchezo wa kikubwa, niliona ujio wake ni kama kuokota dodo chini ya mjohoro.

 

Tuligusanisha ndimi zetu lakini ukweli ni kwamba sikuwa mjuzi sana wa hayo mambo, jambo ambalo hata yeye aliligundua na kumfanya acheke. Basi akawa ni kama ananifundisha kwa vitendo nini cha kufanya, na mimi nikawa mwanafunzi mtiifu mwenye bidii ya kujifunza.

 

“Nataka unitoe upweke ndani ya moyo wangu,” alisema huku akijitoa kwenye mikono yangu, nikamshuhudia akilitoa lile gauni jepesi alilokuwa amevaa, cha kushangaza ni kwamba ndani hakuwa na kitu kingine chochote, kwa hiyo ni kama alijiandaa kuja kunijaribu, wakati msimamo wangu siku zote ni kwamba huwa sijaribiwi.

 

Macho yangu yakatua kwenye kifua chake kilichojaa vizuri, nikalisogeza taulo langu, sasa tukawa saresare maua, macho yake yakatua kwa ‘kiranja mkuu’, akatabasamu na kunitazama.

 

Je, nini kitafuatia? Usikose kesho hapahapa! Unaweza pia kusoma au kusikiliza hadithi nyingine kwa kuingia: www.simulizizamajonzi7113.blogspot.com ,  Facebook: Simulizi za Majonzi au Youtube: Hashpower Online. Usisahau kulike, share na ku-subscribe.

 

 

Leave A Reply