The House of Social Media
gunners X

HII NDIYO ORODHA YA WACHEKESHAJI WAKALI BONGO

KATIKA tasnia ya vichekesho Bongo, kuna vijana wanafanya vizuri mno. Vijana hawa wamekuwa wakionesha vipaji vikubwa na laiti kama tasnia hii ingewekewa mkazo, hawa vijana wangekuwa mbali mno kimataifa!

Hapa chini tunakuletea listi ya wachekeshaji wakali kulingana na tathmini ya uwezo wao wa kuchekesha;

 

1: LUCAS MHUVILE ‘JOTI’

Ukiondoa kizazi cha wazee walioongozwa na aliyekuwa mchekeshaji kinara Bongo, marehemu King Majuto, basi anayemfuatia ni Joti.

Joti alianza kuchekesha mitaani akiwa na Mpoki ndiyo maana likaibuka jina la Mpoki na Joti.

 

Baadaye aliingia kwenye Kundi la Ze Comedy kisha Orijino Komedi. Baada ya kundi hilo kusimama kuruka runingani, sasa Joti anarusha vichekesho vyake mtandaoni kupitia Joti TV na kukamata vilivyo kutokana na uwezo wake wa kujibadilisha kama mtoto, kijana, mzee au mwanamke.

2: EMMANUEL MGAYA ‘MASANJA MKANDAMIZAJI’

Kutoka kwa Joti, uchunguzi wetu ulibaini kwamba anayemfuatia ni Masanja. Masanja alianza kuchekesha takriban miaka 10 iliyopita na amefanikiwa kujipatia umaarufu katika fani hiyo. Mbali na kushiriki katika filamu na vichekesho vya binafsi pia alikuwa mmoja wa memba wa Kundi la Orijino Komedi.

 

Hivi karibuni Masanja amekuwa anaimba muziki wa Injili na ametoa album yake ya Hakuna Jipya. Pia amekuwa akihubiri neno la Mungu na kupewa jina la Street Pastor huku akiendelea kuchekesha na kutupia vipande wa video kwenye mitandao ya kijamii. Kwa sasa ni gumzo na wimbo wake wa ‘Kemea Pepo’.

3: ULIMBOKA MWAKILASA ‘SENGA’

Jamaa ni mkongwe ambaye amefanya filamu kali za komedi zikiwemo Nyama Choma, Jazba, Muuza Mboga, Msela wa Manzese, Kitu Kipya, Shuga Mammy, Nyama ni Nyama, Muuza Genge na nyinginezo nyingi ambazo zimemfanya kukubalika katika tasnia ya vichekesho Bongo na lafudhi yake ya Kinyakyusa.

4: HAJI SALUM ‘MBOTO’

Mboto ni mkali mwingine wa kuchekesha ambaye huwezi kukaa naye kwa dakika moja bila kucheka. Mboto ni Mzaramo wa mkoani Pwani na amefanya vizuri kwenye filamu za kuchekesha ikiwemo Kibajaj na kumjengea jina kubwa hasa anapokuwa mbele ya hadhira.

5: YUSUF KAIMU ‘PEMBE’

Ni kichwa ambacho kimeonesha umahiri wake kwenye filamu kibao zikiwemo Nyama Choma, Version, Gundu, Lakuc-humpa, Moto Bati, Vara-ngati, Jazba, Muuza Mboga, Msela wa Manzese, Shuga Mammy, Nyama ni Nyama, Mganga From China, Back From New York, Madunga Embe, Pedeshee, Waiter, Inye Plus, Inye Gwedegwede, Kijakazi na nyingine nyingi zilizomweka juu vilivyo na lile rungu lake.

6: RASHID MWINSHESHE ‘KINGWENDU’

Kingwendu ni mchekeshaji wa siku nyingi Bongo na ameshiriki katika maigizo mengi ya vichekesho na watu maarufu kama marehemu Mzee Small na Majuto. Kingwendu alishatwaa kemkem za kuwa mwigizaji maafuru wa vichekesho.

6: ISAYA MWAKILASA ‘WAKUVWANGA’

Wakuvwanga ni mchekeshaji aliyepita njia moja na Joti na Masanja kwa maana ya Makundi ya Ze Comedy kisha Orijino Komedi. Baadaye jamaa ambaye naye hupatia kuigiza kama mwanamke alitoa album yake ya muziki iitwayo Kato na sasa anaendelea kurusha vichekesho vyake kwenye mitandao ya kijamii.

7: MUSA KITALE ‘KITALE’

Uchunguzi wetu umebaini kwamba Kitale amefanya vizuri kwenye filamu za komedi za Chizi Kalogwa Tena, 4 Days Mission, Sina Jinsi, Mkweli Nani, Dini Imani, Msela, Utani, Zungusha, Bwege Mtozeni, Break Down na nyingine kibao.

8: TATU YUSUF ‘ASHA BOKO’

Ni mmoja wa waigizaji wa wanawake wenye kuvunja mabavu akiringia umbile lake kubwa na kipaji halisi cha sanaa alichonacho.

Amedumu kwenye fani hiyo kwa zaidi ya miaka 10 tangu alipoanza kutamba na Kundi la Kaole Sanaa.

Amefanya filamu za vichekesho za Kizungunguzu, Shoe Shine, Street Girl, Boss, Teja, Karaha, Ngekewa na nyingine nyingi.

9: SILVESTER MJUNI ‘MPOKI’

Alianza kuigiza na Joti mitaani kisha akapita kwenye Makundi ya Ze Comedy na Orijino Komedi. Baada ya Orijino Komedi kusimama kurusha kipindi chake kupitia Televisheni ya TBC1, Mpoki alihamia kwenye utangazaji katika Kituo cha Redio EFM huku akiendelea kufanya vichekesho vya majukwaani kwa kutumia misemo ya Kiswahili inayoibuka mitaani.

10: STEVEN MENGERE ‘STEVE NYERERE’

Steve alianza kuchekesha kwa kuiga sauti za watu maarufu akiwemo Hayati Mwalimu Nyerere. Baadaye aliingia kwenye filamu za vichekesho kama Mwalimu Nyerere kabla ya kujikita kwenye kuchekesha majukwaani.

Ijumaa Wikienda

GIGY MONEY; Mimi ni mzuri wanaume wanapagawa/ Cardi b ameniiga

Comments are closed.