WINGU la simanzi limetanda kijiji cha Makundi kaunti ya Machakos nchini Kenya baada ya jamaa mmoja wa miaka 28 kumuua mamake wa miaka 70 na mpwa wake kwa kupika mayai yake ilhali alikuwa hanunui chakula.
Hilo limetokea Januari, 28, 2020, jamaa huyo alipomshambulia kwa panga mamake huku dadake na mpwa wake wakikimbia na alipowapata alimkata dadake mguu kabla ya kumuua mpwa wake.
Dadake mshukiwa anapokea matibabu katika hospotali ya Machakos Level Five baada yake kumkata mguu wakati wa kisa hicho.
Majirani walifichua kwamba jamaa alikuwa mtundu na kwa wakati mmoja alimchinja mbuzi wa mamake, akampika, akamla na kisha baadaye kuwapia mbwa mabaki wa nyama hiyo.
Waliongeza kuwa alikuwa na mazoea ya kuwachinja kuku wa mamake na kila alipoulizwa alizua vurugu. Wenyeji sasa wanaishi kwa hofu kwani wana wasiwasi huenda mshukiwa akawashambulia wanao wakielekea shuleni.
Polisi wanamsaka mshukiwa ambaye anasemakana yuko mafichoni baada ya kisa hicho kuripotiwa katika kituo cha polisi cha Katheke.