The House of Favourite Newspapers
gunners X

Kesi ya Mange Kimambi Yaaahirishwa Hadi Januari 2026 – Sababu Ni Upelelezi Haujakamilika

0

Kesi ya Uhujumu Uchumi namba 000021172 ya mwaka 2025, inayomkabili Mwanaharakati Mange Kimambi imeahirishwa mpaka Januari 28, 2026 baada ya upande wa serikali kuieleza mahakama kuwa upelelezi wa shauri hilo haujakamilika.

Leo Disemba 04, 2025 shauri hilo liliitwa mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Hassan Makube ambapo upande wa Jamhuri uliieleza mahakama kuwa upelelezi bado hivyo ukaomba shauri kupangiwa tarehe nyingine.

Upande wa Mange Kimambi haukuwa na Wakili wa utetezi hivyo Hakimu Makube akauagiza upande wa Jamhuri kuhakikisha taratibu zote zimekamilika ili tarehe hiyo ikifika shauri lianze kusikilizwa.

Mange Kimambi anakabiliwa na mashtaka ya utakatishaji wa fedha kiasi cha Shilingi milioni Sh138.5 ambapo inadaiwa kuwa kati ya Machi 1 na Machi 31, 2022, katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam, Mange alijipatia Sh138.5 milioni akifahamu kuwa fedha hizo ni zao la uhalifu. Inadaiwa pia alizipata fedha hizo kwa kufanya kazi ya uandishi wa habari bila kibali pamoja na kuzidai kwa vitisho.

Shtaka hilo linaangukia kifungu 12(1)(d) na 13(a) cha Sheria ya Utakatishaji Fedha Sura ya 423 ya mwaka 2019, ikisomwa sambamba na Sheria ya Uhujumu Uchumi.

Asubuhi ya Desemba 2, 2025, video iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii ilimuonesha Mange akithibitisha kuwa amepokea taarifa kuhusu kufunguliwa kwa kesi hiyo, akidai kuwa Serikali ya Tanzania imedhamiria kumrejesha nchini.

Sheria ya kurejeshwa kwa watuhumiwa kutoka nje ya nchi (Extradition Act, 2019) inatambua utakatishaji fedha kama moja ya makosa yanayoweza kupelekea nchi kuomba mtuhumiwa kurejeshwa.

Hatua hiyo mpya inakuja takribani mwezi mmoja baada ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Hamza Johari, kueleza kuwa ofisi yake inaangalia uwezekano wa kumchukulia hatua Mange kutokana na tuhuma za kuhamasisha maandamano.

Akizungumza muda mfupi baada ya kuapishwa katika wadhifa huo jijini Dodoma, Johari alisema Serikali inatumia mikataba ya ushirikiano kati ya Tanzania na Marekani kutathmini uwezekano wa kumrejesha nchini.

MAMA TERRY AJILIPUA KUHUSU GEN – Z – ”NIMEZIKA WANANGU WAWILI – NAJUA UCHUNGU – NISIJE NIKATEKWA”

Leave A Reply