Kizazi cha Gen-Z Chatajwa na Kagame Kama Changamoto Mpya kwa Serikali Afrika

Rais wa Rwanda, Paul Kagame, amesema kuwa Bara la Afrika linaweza kushuhudia wimbi jipya la mapinduzi endapo viongozi wake hawatashughulikia changamoto zinazowakabili wananchi, hususan vijana wa kizazi kipya (Gen-Z) ambao wanaonyesha kiu ya mabadiliko ya haraka.
Akizungumza kufuatia matukio ya karibuni ya mapinduzi Madagascar mwezi uliopita na sintofahamu ya kisiasa Guinea-Bissau tangu Jumatano, Kagame amesema Bara la Afrika limekumbwa na historia ndefu ya mapinduzi—takribani 130 katika nchi 36 tangu mwaka 1952 na karibu mapinduzi 10 katika kipindi cha miaka mitano iliyopita pekee.
Kagame alieleza kuwa kabla ya kulaumu mapinduzi yanayotokea, viongozi wanapaswa kujiuliza sababu za msingi zinazosukuma jeshi au wananchi kutaka kubadilisha mamlaka kwa nguvu. Alikiri kuwa nchi nyingi za Afrika, ikiwemo Rwanda yenyewe, zimekumbwa na changamoto mbalimbali zinazohusiana na uongozi, ukosefu wa uwajibikaji, na kutosikiliza matakwa ya wananchi.
Amesema kuwa vijana wa kizazi kipya, maarufu kama Gen-Z, wanaongezeka kwa kasi na hawasubiri tena miaka mingi kuona mabadiliko. Kwa maoni yake, kundi hilo linaweza kuwa chanzo kingine cha mapinduzi endapo mazingira ya kiuchumi, kijamii na kisiasa hayataboreshwa.
Kagame alisisitiza kuwa njia pekee ya kuzuia mapinduzi ni viongozi kubadilika, kusikiliza wananchi na kushughulikia changamoto zinazochochea hasira, hali ngumu ya maisha na kukosekana kwa usawa.
“Afrika ina matatizo mengi. Lakini namna viongozi wanavyoendesha nchi zao ndiyo mara nyingi husababisha hali inayowafanya wananchi kutafuta njia mbadala, ikiwemo mapinduzi,” alisema Kagame.
Kauli hii imezidi kuibua mjadala mpana kuhusu mustakabali wa demokrasia na uongozi barani Afrika, hasa wakati huu ambapo misukosuko ya kisiasa na kiuchumi imeendelea kuongezeka.

