The House of Favourite Newspapers

Kuwahi Kupoteza Uwezo wa Kuzaa kwa Mwanamke

TATIZO hili linaambatana na mwanamke kukoma uzazi kabla ya muda wake, yaani anazeeka mapema. Mwanamke mwenye tatizo hili hupatwa na tatizo kubwa la mfumo wa vichocheo mwilini ambapo husababisha kusinyaa kwa mfumo mzima wa uzalishaji mayai. 

Kwa kawaida kazi ya vifuko vya mayai ni kuzalisha mayai na homoni. Katika tatizo hili vifuko vya mayai hushindwa kuzalisha homoni au kichocheo cha Estrogen ambacho ni kichocheo cha kike na kudhoofisha vichocheo vya uzalishaji mayai hivyo kufanya mayai yasizalishwe. Tatizo hili huwapata zaidi wanawake walio katika umri wa kuzaa na chini ya miaka arobaini.

CHANZO CHA TATIZO

Kama tulivyoona, tatizo huwatokea wanawake walio na umri chini ya miaka arobaini na ambao huhangaika kutafuta watoto au ujauzito kwa muda mrefu lakini hawafanikiwi. Kuna vyanzo vikuu vinne vya tatizo hili kama tutakavyovitaja. Kwanza ni tatizo liitwalo ’Enzyme defects’.

Hapa mwanamke huwa na tatizo la kutoa maziwa kwenye matiti yake pasipokuwa na mimba wala kunyonyesha wala historia ya kuharibikiwa na mimba. Chanzo cha pili ni ‘Genetic difect’. Hili ni tatizo la kurithi na la kuzaliwa nalo, linahusiana zaidi na vinasaba vyake vya mfumo wa uzazi mfano kuwa na viungo vidogo vya uzazi hasa vifuko vya mayai kuonesha vimesinyaa na mwanamke huyu hana historia ya kuvunja ungo.

Pia msisimko wa mwili unakuwa hafifu hata misuli yake ya mwili haipo imara na umbile lake huwa haliwi kama wasichana wengine wa kawaida, hana matiti na pia hana nywele kwapani na sehemu zake za siri ingawa umri wake unakuwa mkubwa. Tatu ni matatizo katika mfumo wa kinga mwilini. Hili linasababishwa na magonjwa makali yanayoathiri moja kwa moja mfumo wa kinga mwilini kama kisukari, upungufu wa damu mara kwa mara, fangasi sugu katika mifumo ya wazi mwilini kama kinywani na sehemu za siri.

Mengine kitaalamu ni ‘Thyroiditis, Adisson disease, magonjwa ya mishipa ya fahamu na misuli na mengine mengi. Tatizo la nne ni linalohusiana na mfumo wa mazingira kwa ujumla. Tatizo hili linahusiana na matumizi ya dawa kali za kutibu kansa, uvutaji wa sigara, mionzi ya x-ray katika viungo vya uzazi mfano endapo mwanamke atafanyiwa x- ray katika maeneo ya nyonga basi
inashauriwa maeneo ya ovari yafunikwe na vifaa maalumu kuzuia mionzi.

Kingine ni maambukizi sugu ya virusi mwilini. Mwanamke mwenye matatizo yote haya manne mwisho wa siku yupo hatarini kupata saratani ya vifuko vya mayai.

DALILI ZA UGONJWA

Mwanamke mwenye tatizo hili huweza kupatwa na mojawapo au dalili hizi zifuatazo; Kutokupata hedhi ‘Amenorrhoea’. Hii ni kutovunja ungo au ana historia kwamba alishawahi kupata damu ya hedhi lakini sasa ni muda mrefu  hajapata tena. Dalili nyingine ni kuvurugika kwa mfumo wake wa hedhi, yaani hajui mwenendo wa siku zake, yaani mwezi anapata na mwingine hapati hivyo hata kupata ujauzito inakuwa vigumu.

Hupatwa na upungufu mkubwa wa homoni ya kike ambayo ni Estrogen hivyo kufanya alalamike mara kwa mara maumivu ya nyonga, kiuno, mgongo, mabega na magoti, mifupa huwa myepesi na laini na akianguka kidogo anavunjika. Uke unakuwa mkavu na hulalamika tatizo la muwasho ukeni mara kwa mara na maumivu wakati wa kujamiiana. Hamu ya kushiriki tendo la kujamiiana pia hupotea.

UCHUNGUZI

Hufanyika katika kliniki za magonjwa ya akina mama na matatizo ya uzazi kwenye hospitali za mikoa ambapo vipimo vya damu, kupima homoni vitafanyika. Uchunguzi wa kina hufanyika zaidi kwa wanawake wenye matatizo haya ambao wana umri chini ya miaka arobaini ambao wanahitaji kupata ujauzito.

TIBA NA USHAURI

Matibabu yatazingatia uchunguzi lakini jambo kubwa ni kwamba mgonjwa atapatiwa dawa za homoni na kurekebisha mzunguko wa hedhi na mfumo wa uzazi. Wahi hospitali kwa uchunguzi na tiba.

Comments are closed.