The House of Favourite Newspapers

Kwa nini wachumba wanakupiga kibuti kila mara?

UHUSIANO wa kimapenzi kwa vijana wengi hukumbwa na changamoto nyingi. Zipo sababu kadhaa zinazosababisha hilo, lakini kubwa zaidi ni ugeni wa mambo ya mapenzi na kutokupata elimu sahihi juu ya maisha ya urafiki na uchumba kabla ya ndoa. 

 

Ni wazi kuwa kama uhusiano wa urafiki na baadaye uchumba hautakuwa mzuri, basi kuna uwezekano mkubwa wa ndoa kutokuwa imara. Hii ndiyo sababu gazeti lako bora la Amani kuamua kukusogezea safu hii ili uweze kupata elimu kuhusu uhusiano katika kipindi cha ujana.

 

Nitakuwa hapa kila Alhamisi na mada mbalimbali zitakazokubadilisha fikra zako. Leo katika ufunguzi, tunaangalia sababu za baadhi ya wadada kupigwa kibuti. Naamini umekutana na kesi hizo mara nyingi. Ama kwako mwenyewe au kwa rafiki zako.

 

Marafiki, mapenzi yamegawanyika katika sehemu mbili zisizo rasmi – maumivu na furaha. Kupata mateso au furaha katika uhusiano inategemea zaidi na wewe, jinsi ulivyoanzisha uhusiano huo, unavyoulea na hata staili unayoishi na mpenzi wako.

 

Je, wewe uhusiano wako ukoje? Umekuwa kwenye migogoro ya mara kwa mara na wavulana unaokuwa nao kwenye uhusiano na hatimaye kuachana? Imekuwa bahati kwako kukutana na mada hii. Tuangalie sababu zinazoweza kusababisha kuachwa mara kwa mara.

 

KUMWCHIA KILA KITU

Hi ni kasoro ya kwanza, wasichana wengi hawafahamu kuwa hiki ni kikwazo katika zama hizi za Sayansi na Teknolojia. Unapokuwa mtu wa mizinga kila siku, unadhani mwanaume huyo atakuvumilia? Zamani hizo mambo haya yalikuwa yanawezekana, mwanaume anakuwa kila kitu ndani ya nyumba, lakini katika kipindi hiki kinachoitwa ‘haki sawa’ lazima familia isaidiane.

 

Mwanaume wa sasa anayesaka mke bora wa kuoa, kati ya vipengele muhimu anavyoangalia ni pamoja na mpenzi huyo anayetarajia kuwa mkewe awe na future ya maisha. Sasa kama kila akikutana na wewe unampiga vizinga unadhani anaweza kukubali kuendelea na wewe? Hakika hawezi na kama akiendelea na wewe ujue huyo atakuwa na nia ya kustarehe tu na wewe, siku moja hamu yake ikiisha atakutosa!

 

Huna sababu ya kusubiria siku hiyo, unachopaswa kufanya ni kufanya mabadiliko ya haraka katika maisha yako! Unajua ni nini? Mwanaume huyo atakuona una busara sana ikiwa utamwomba akulipie ada kwa ajili ya kusoma kozi fulani au utakapomuomba mtaji wa kufungua biashara kuliko kuishia kuwa mtu wa vizinga kila siku.

 

Fahamu kuwa hakuna mwanaume anayependa kuwa na mwanamke tegemezi. Ndiyo maana wakati mwingine, baadhi ya vijana wa kiume huamua kuoa wanawake wanaowazidi umri kwa kuzingatia vipato. Unajua kwa nini? Kwa sababu wanaangalia maisha yao ya baadaye, upo hapo?

MAJIBU MABOVU

Hili nalo ni tatizo katika uhusiano, tatizo hili linatosha kabisa kukukosesha mpenzi wa kudumu ambaye baadaye anaweza kuwa mchumba na hatimaye kuingia katika ndoa. Jichunguze vizuri je, wewe ni mkorofi? Unamjibu hovyo mpenzi wako?

 

Unaufahamu vipi ukorofi? Hapa tunazungumzia dharau, majibu ya mkato na kutokuwa msikivu. Mwanamke makini ambaye anatarajia kuingia katika ndoa hapo baadaye na mchumba wake lazima atakuwa makini na ulimi wake, hawezi kumjibu vibaya mpenzi wake kwa kuwa anajua kuwa anamjibu mumewe mtarajiwa.

 

Jichunguze vizuri, utagundua kuwa kuna tatizo hili katika uhusiano wako uliopita. Ukorofi mwingine ninaozungumzia hapa ni kumpangia mwenza wako muda wa kuwa naye faragha, akikuhitaji muda fulani unamkataa na kutoa sababu kibao zisizo na msingi, huu ni ukorofi, ni sawa na kumruhusu mpenzi wako atafute mwanamke mwingine nje.

 

Akishaenda huko na hivi wadada wa kileo walivyo hodari, utampata wapi tena? Itakuwa imetoka hiyo! Kwa leo naweka kituo kikubwa hapa, usikose Alhamisi ijayo katika sehemu ya mwisho ya mada hii. Unajua nini? Baada ya mada hii, nitazungumza na wakaka.

 

TUWE PAMOJA MARAFIKI!

Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Uhusiano anayeandikia Magazeti ya Global Publishers. Ameandika vitabu vingi, vikiwemo True Love, Let’s Talk About Love na Maisha ya Ndoa vinavyopatikana kwa oda. Kwa sasa anaandaa kitabu chake kipya cha SIRI ZA NDOA YENYE FURAHA kitakachotoka hivi karibuni.

Comments are closed.