Kwagilwa Aagiza Kusitisha Malipo Ya Mhandisi Mshauri Aliyechelewesha Mradi Wa Daraja Tabora

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI) anayeshughulikia Elimu, Reuben Kwagilwa (Mb), ameagiza kusitishwa malipo yote ya Mhandisi Mshauri Advanced Engineering Solution Ltd kutokana na kushindwa kusimamia ipasavyo ujenzi wa daraja katika barabara ya Ndevelwa, Manispaa ya Tabora.
Agizo hilo amelitoa leo Januari 06 2026 kwa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) mkoa wa Tabora, wakati wa ziara yake ya ukaguzi wa mradi huo unaotekelezwa kupitia Mpango wa Uboreshaji wa Jiji la Dar es Salaam Awamu ya Pili (DMDP-II) kupitia kipengele cha Contingent Emergency Response Component (CERC).

Mhe. Kwagilwa amesema kuwa Mhandisi Mshauri huyo ameshindwa kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa mkataba, hali iliyosababisha ucheleweshaji wa mradi pamoja na kukosekana kwa ufuatiliaji wa karibu kwa mkandarasi anayeendelea na ujenzi wa daraja hilo muhimu kwa mawasiliano ya wakazi wa eneo hilo.
“Hii barabara ni ya kwetu. Tumemuagiza huyu amsimamie mkandarasi, lakini mkandarasi hayupo kazini na anajua ninakuja. Sasa naelekeza, sitisheni malipo kwa Mhandisi Mshauri hadi tutakapojiridhisha na kazi anayoifanya.
Acheni kuweka maneno maneno kwenye kazi za Watanzania,” amesisitiza.

Ujenzi wa daraja hilo umefikia takribani asilimia 70 na unagharimu Shilingi Milioni 58.7, na unatarajiwa kukamilika ifikapo Februari 2026 endapo usimamizi thabiti utaimarishwa katika hatua zilizobaki.
Mhe. Kwagilwa amehimiza kuwa Serikali haitavumilia uzembe wa aina yoyote kutoka kwa wasimamizi wa miradi ya maendeleo, kwakuwa ucheleweshaji wa miradi huathiri utoaji wa huduma kwa wananchi na matumizi sahihi ya fedha za umma.


