The House of Favourite Newspapers
gunners X

Bilioni 1.6 za Tozo Zapelekwa Morogoro – Video

0

SERIKALI imesema Mkoa wa Morogoro umepata Shilingi Bilioni 1.637 za Tozo ya Miamala ya Simu kwa ajili ya kujenga vituo vya afya 5 (Itete, Iragua, Uchindile, Nongwe na Mkuyuni Tomondo) na pia kumalizia maboma ya shule 111.

 

Hayo yamesemwa leo Oktoba 02, 2021 na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa,wakati akizungumza na wanahabari mkoani humo kuhusiana na masuala mbalimbali yahusuyo serikali.

 

“Hali ya Mkoa wa Morogoro ni shwari, ulinzi na usalama upo imara na wananchi wanaendelea kuchapa kazi zao za kujipatia kipato na ujenzi wa Taifa kama kawaida. 

 

“Fedha za tozo ya miamala ya simu hapa Morogoro tumeshaleta bilioni 1.637 na zinaenda kujenga vituo vya afya 5 na kumalizia maboma ya shule 111, tumeamua tuweke wazi kuhusu fedha hizi wananchi wajue haziendi kwenye mfuko wa Msigwa.

“Serikali inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu imeendelea kutoa fedha za kugharamia huduma za kijamii kama vile maji, barabara, afya, umeme na miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa hapa Morogoro. Bilioni 75.322 za maendeleo zimeletwa Morogoro.

 

“Serikali imeleta TSH Bilioni 21.776 kwa ajili ya kutekeleza mradi wa kuongeza uzalishaji na tija kwa zao la mpunga hapa Morogoro, Yaani kujenga na kukarabati miundombinu ya umwagiliaji na kujenga maghala.

 

“Serikali kwa kushirikiana na wadau, imeweka mkakati wa kuongeza uzalishaji wa sukari nchini na hapa Morogoro kuna viwanda 3 vinavyotegemewa.

“Kule Kilombero ambapo Serikali ina hisa za 25% katika kiwanda cha Ilovo, kuna kazi kubwa inaendelea ya upanuzi wa kiwanda hiki ili kiongeze uzalishaji wa sukari kutoka tani 130,000 zinazozalishwa kwa mwaka hivi sasa hadi kufikia tani 260,000.

“Kiwanda cha Mbigiri ambako Shirika letu la NSSF na Jeshi la Magereza wamewekeza, tunatarajia kiwanda hiki kianze kuzalisha tani 50,000 kuanzia Julai au Agosti 2022. Kule Malinyi kuna uzalishaji wa zao la Kakao, Serikali imeandaa mpango kabambe wa kuhakikisha zao hili linazalishwa kwa wingi hapa Morogoro kama ilivyo kule Mbeya.

“Najua wengi watakuwa na shauku kubwa ya kutaka kujua kuhusu uimarishaji wa barabara ya Morogoro – Dodoma. Nafurahi kuwaambia kuwa Serikali imeanza mchakato wa kuijenga upya barabara hii. Serikali inakwenda kutekeleza mradi huu mkubwa kwa kutambua kuwa hii ni barabara muhimu kwa nchi yetu (Morogoro-Dodoma).

 

“Hivi navyozungumza anatafutwa mkandarasi mshauri kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina. Lengo la Serikali ni kupanua barabara hii kwa kuwa na njia nne (mbili za kwenda na mbili za kurudi).

“Hii ndio barabara inayotumika kusafirisha mizigo mingi inayokwenda katika Kanda ya Kati, Kanda ya Ziwa na Kanda ya Magharibi. Hii barabara ndio inayotumika kusafirisha mizigo inayokwenda katika Nchi jirani za Rwanda, Burundi, Uganda, Congo (DRC) na Sudan Kusini,” amesema Msigwa.

 

Leave A Reply