Rais Samia Ahutubia Bunge kwa Mara ya Kwanza – Video
Ikiwa Watanzania 8,224,271 pekee ndiyo wenye uhakika wa matibabu nchini, Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema mipango na mikakati inawekwa ili kila mmoja awe na uhakika wa kutibiwa kwa kuimarisha mifuko ya bima za afya.
Samia ameyasema hayo leo Alhamisi Oktoba 22, 2021 wakati akilihutubia Bunge la Tanzania ikiwa ni hotuba yake ya kwanza tangu kuapishwa kushika wadhifa huo Machi 19, 2021.
“Tutaimarisha mifuko ya bima ya afya ili kufikia bima ya afya kwa Watanzania wote. Kwa sasa inasikitisha Watanzania 8,224,271 ndiyo wanatumia bima ambao ni asilimia 14 tu, tutahamasisha ujenzi wa viwanda vya kutengeneza dawa, vifaa tiba na vitendanishi,” amesema.
Amesema Serikali yake imekusudia kuimarisha na kuboresha huduma ya jamii ikiwemo huduma za kupunguza vifo vya wajawazito na watoto.
“Wabunge huu ni mradi wangu wa moyoni kabisa nilipokuwa makamu wa rais nilizindua mradi wa jiongeze tuwavushe salama.”
“Binafsi huwa ninasikitika sana ninapoona kinamama wanafariki wakijifungua suala linaloweza kuzuilika ile kampeni imefanikisha kupunguza vifo,” amesema.
Katika hotuba yake amegusia kupambana na magonjwa yasiyoambukiza, matibabu ya kibingwa, kuimarisha utoaji wa huduma kwa wazee na wataweka mipango maalum kuhudumia makundi ya magonjwa adimu.
Amesema wakati kamati aliyoiunda na corona ikiendelea na kazi amewataka Watanzania kuchukua tahadhari zote, “Kila mmoja awajibike ulinzi wa afya yako unaanza na wewe mwenyewe.”