Makamu wa Rais Nchimbi Aongoza Mazishi ya Jenista Mhagama Ruanda – Mbinga (Picha +Video)

Makamu wa Rais wa Jam huri ya Muungano wa Tanzania, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi amewaongoza waombolezaji kwenye Mazishi ya aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Peramiho, Marehemu Jenista Mhagama, yaliyofanyika katika Kijiji cha Ruanda Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma leo tarehe 16 Desemba 2025.
Akitoa salamu za rambirambi mara baada ya mazishi hayo, Makamu wa Rais amesema marehemu Jenista Mhagama alikuwa mtumishi wa kweli wa watu wake ambaye aliwatumikia na kuwajali.
Amesema Serikali, Wananchi na Chama cha Mapinduzi, wamepoteza mtu muhimu ambaye mchango wake hautasauhaulika katika nyadhifa mbalimbali ambazo amewahi kutumika.

Makamu wa Rais ameongeza kwamba Serikali na Chama Cha Mapinduzi itaendelea kuenzi mchango wa marehemu Jenista Mhagana kwa kuendelea kuwa watetezi wa wananchi wa chini, ambapo ametoa wito kwa Viongozi wa Serikali kuhakikisha wananchi wa hali ya chini ndio wanakuwa kipaumbele chao cha kila siku.
Aidha Makamu wa Rais amewasilisha salamu za shukrani za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alizozitoa kwa familia na wananchi wa Ruvuma kwa ujumla kutokana na maisha ya marehemu Jenista Mhagama. Amesema Rais Dkt. Samia ameguswa sana na msiba huo kutokana na mchango aliotoa marehemu Jenista Mhagama enzi za uhai wake.
Pia amewashukuru Viongozi wa Kanisa ambao wameshiriki katika Ibada mbalimbali zilizofanyika za kumuombea marehemu Jenista Mhagama kuanzia mkoani Dodoma hadi mkoani Ruvuma.


