Mobetto na Aziz Ki Waweka hadharani Uhusiano Wao – Picha

KIUNGO mshambuliaji wa klabu ya Yanga SC, Stephanie Aziz Ki, pamoja na mwanamitindo, muigizaji, na msanii wa muziki wa kizazi kipya nchini Tanzania, Hamisa Mobetto, hatimaye wameamua kuweka hadharani uhusiano wao wa kimapenzi baada ya kuwa kwenye mahusiano ya siri kwa muda mrefu.
Kwa muda mrefu, wawili hao walikuwa wakikanusha uvumi wa kuwa pamoja, huku wakiepuka kujibu maswali ya mashabiki na vyombo vya habari kuhusu ukaribu wao. Hata hivyo, sasa si siri tena baada ya wawili hao kushiriki picha za pamoja wakifurahia mapumziko ya kifahari (vacation) nchini Dubai.
Picha hizo zilizosambaa mitandaoni zilionyesha wawili hao wakiwa kwenye mandhari ya kuvutia, wakiwa wenye furaha na upendo mkubwa. Mbali na picha, wawili hao walichapisha jumbe za kimahaba kupitia kurasa zao za Instagram, zikionyesha wazi hisia zao za dhati.

Hamisa Mobetto, kupitia ukurasa wake wa Instagram, aliandika maneno yenye hisia kali akisema, “He is exactly the poem that I want to write,” akionyesha namna anavyompenda Stephanie Aziz Ki.
Kwa upande wake, Stephanie naye hakuachwa nyuma, kwani alijibu kwa maneno matamu yaliyoashiria mapenzi yao yamefika hatua ya juu zaidi.
Mashabiki na wafuasi wao mitandaoni wamepokea habari hizi kwa hisia tofauti; baadhi wakifurahia na kuwatakia kila la heri, huku wengine wakishangazwa na uhusiano huo ambao ulifanikwa kufichwa kwa muda mrefu. Bila shaka, mapenzi kati ya wawili hao sasa yamepamba moto, na safari yao ya kimapenzi inazidi kushamiri mbele ya macho ya dunia.

