The House of Favourite Newspapers

Mbeya: Aliyeoa Yatima Mlemavu Gumzo, Wanavyoishi Utashangaa! – Video

 

WAKATI wanandoa wasiyokuwa na ulemavu hata wa kidole gumba wakiishi maisha ya kutwangana makonde na kununiana, hali ni tofauti kwa kijana Timotheo Mwazembe aliyeoa mlemavu.

 

Maisha ya ndoa ya Timotheo (29), mkazi wa Ilemi jijini Mbeya aliyemuoa Salome Msomba (30) ambaye ni mlemavu yamekuwa gumzo kwa jinsi kijana huyo anavyompenda na kumheshimu mkewe.

 

Taarifa za wengi kushangazwa na ndoa hiyo zilipozidi kusambaa, Risasi Jumamosi likaona ni vyema kuitembelea familia hiyo iliyobahatika kupata mtoto wa kiume hivi karibuni ili kujua mawili matatu kuhusu maisha yao.

Akizungumza na Risasi Jumamosi, Timotheo alisema anajisikia fahari kuishi na mkewe ambaye ni mlemavu licha ya kupata vikwazo vingi kutoka kwa ndugu zake.

“Mimi na Salome tulikutana katika Kijiji cha Nanyala Wilaya ya Mbozi Mkoa wa Songwe nilipokuwa nafanya biashara ya kuuza mayai.

“Mtu ambaye nilikuwa namtegemea kunikusanyia mayai ni Salome, ndipo tukaanza urafiki mpaka hivi tumekuwa mume na mke,” alisema Timotheo.

 

Siku zote mapenzi ni mafuriko, huwezi kuyazuia kwa mikono; ndivyo ilivyokuwa kwa kijana huyo ambaye aliamua kuziba masikio asisikie kelele za ndugu na marafiki zake waliokuwa wakimuwekea pingamizi la kumuoa Salome kwa sababu ya ulemavu wake.

 

“Mwanzo tulikuwa tukiona kama Timotheo siyo wa kawaida lakini kwa jinsi wanavyoishi maisha ya furaha na kupendana wanatupa funzo kubwa katika maisha ya ndoa.

“Mimi nawaombea mema sana kwa Mungu, azidi kuwabariki na kuyafanya mepesi maisha yao,” alisema Samson kijana aliyejitambulisha kuwa ni rafiki wa Timotheo.

Kwa upande wake Salome akielezea historia fupi ya maisha yake alisema alipata elimu ya msingi, Katumba Wilaya ya Rungwe Mkoa wa Mbeya.

“Wakati nasubiri matokeo nilifiwa na wazazi wangu wote na kubaki yatima.

“Baada ya hapo alinichukua mama mdogo aliyekuwa akiishi eneo la Igurusi ambako nilifaulu kwenda kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari ya Jangwani Mkoa wa Dar es Salaam,” alisema Salome.

 

Aliongeza kuwa kutokana na mama yake mdogo kukosa fedha za kumsomesha alishindwa kuendelea na masomo.

Aidha alidai kuwa mama yake huyo alimshauri kurudia darasa la sita jambo ambalo hakulikubali hivyo kutakiwa na mama yake kuondoka na kwenda kuishi Itumba Ileje Mkoa wa Songwe.

Akiendelea na maisha Itumba, Salome anadai alitengwa na ndugu kwa madai kuwa amekataa kusoma na hivyo kuonekana kama mzigo wa familia.

“Maisha ya machungu yalipita, Mungu akanipatia Timotheo ambaye kusema kweli tunapendana na mtoto wetu tumempa jina la Emmanuel, hadi sasa ana miezi mitatu,” alisema Salome.

Kuhusu kukabiliana na changamoto za maisha, Salome alisema amekuwa akijishughulisha na uuzaji wa mkaa huku mumewe akifanya shughuli za udobi.

Pamoja na kuwepo kwa maisha ya furaha katika maisha yao, mwandishi wetu alishuhudia baadhi ya changamoto ambazo wanandoa hao wanakabiliana nazo.

 

Mfano katika kipindi hiki Timotheo amekuwa mstari wa mbele kusaidia malezi ya mtoto na kukosa muda wa kwenda kutafuta mahitaji ya familia.

Aidha, ukosefu wa baiskeli ya wenye ulemavu nayo ni tatizo ambalo linamlazimu Timotheo anapotaka kuongozana na mkewe kumpakiza kwenye baiskeli ya kawaida huku akiwa amembeba mtoto mgongoni.

Kutokana na changamoto hizo gazeti linawaomba wasamaria wema kujitokeza kuisaidia familia hiyo kwa hali na mali ili izidi kuwa na furaha na kujijenga zaidi kimaisha.

STORI: Ezekiel Kamanga, MBEYA.

 

TAZAMA HAPA VIDEO YA WANANDOA HAO

Comments are closed.