The House of Favourite Newspapers
gunners X

Mfahamu Azzan Zungu Spika wa Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

0
Mussa Azzan Zungu ndiye Spika mpya wa Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mussa Azzan Zungu ndiye Spika mpya wa Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mwaka 2025 mpaka 2030. Ni kiongozi mwenye uzoefu mkubwa katika siasa na utumishi wa umma.

Zungu Novemba 11, 2025, alichaguliwa kuwa Spika wa Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, baada ya kupata kura 378 kati ya kura 383 zilizopigwa na wabunge wa Bunge la Tanzania.

Uteuzi wake ulifanyika kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), huku Spika aliyekuwepo , Dk. Tulia Ackson, akijiondoa kwenye kinyang’anyiro hicho bila kuelezwa sababu za msingi kufanya hivyo.

Zungu aliandika historia kwa kuchaguliwa kuwa spika wa Bunge la Tanzania kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) akifuata nyayo za viongozi mashuhuri waliowahi kushika wadhifa huo kama Adam Sapi Mkwawa, Pius Msekwa, Samuel Sitta, Anna Makinda, Job Ndugai na Dk. Tulia Ackson.

Zungu alianza safari yake ya kielimu katika Shule ya Msingi St. Joseph’s (sasa inaitwa Forodhani) jijini Dar es Salaam kati ya mwaka 1958 na 1965. Baada ya hapo aliendelea na masomo ya sekondari katika Shule ya Kinondoni Muslim (1966-1967) na baadaye Shule ya Tambaza (1968-1969).

KUSHIRIKI SIASA
Akiwa mwanafunzi, alianza kushiriki katika shughuli za kisiasa kupitia chama cha TANU, ambapo aliongoza tawi la chama shuleni.
Baada ya masomo ya sekondari, Zungu alihamia Toronto, Canada, ambako alisomea stashahada ya ufundi wa vyombo vya anga na urubani.

Alifanya kazi nchini humo kama mhandisi wa ndege hadi mwaka 1982, kisha akaendelea kufanya kazi katika Falme za Kiarabu hadi mwaka 1993 kabla ya kurejea nyumbani Tanzania.

Zungu alirejea rasmi kwenye siasa mwaka 2000, ambapo alichaguliwa kuwa diwani wa Kata ya Mchikichini kupitia CCM, ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Ilala. Mwaka 2003 aliteuliwa kuwa Naibu Meya wa Ilala.
Mwaka 2005 alichaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Ilala, nafasi aliyoendelea kuishikilia kwa vipindi vitano mfululizo hadi mwaka 2025.

Akiwa Bungeni Zungu amewahi kushika nyadhifa mbalimbali ikiwemo: Naibu Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje (2007-2011), Mwenyekiti wa Umoja wa Wabunge wa Jumuiya ya Madola (CPA) -Tanzania, alikuwa Naibu Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Jamii (2015-2018)

Baadaye akawa Mwenyekiti wa Bunge katika vipindi vya 2012 na 2016. Mwaka 2020, aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), nafasi aliyohudumia hadi mwisho wa kipindi cha Bunge la 12.

Kufuatia kujiuzulu bila maelezo ya kutosha kwa Spika Job Ndugai, Zungu alichaguliwa kuwa Naibu Spika, kabla ya kupanda ngazi hadi kuwa Spika wa Bunge la 13 mwaka 2025 baada ya aliyekuwa Spika Dkt Tulia Ackison kuondoa fomu yake ya kugombea nafasi hiyo baada ya awali kuonesha nia ya kuwania tena nafasi yake.
Watanzania wanasubiri kuona misimamo yake kisiasa ili waone utofauti wa kimaamuzi ikilinganishwa na maspika waliopita. Ngoja tuone.

Stori na Elvan Stambuli | GPL

MAHAKAMA KUU YAPINDUA MEZA! SIKU 106 ZAWAGHARIMU WALALAMIKAJI – HAPA NDIPO CHADEMA WALIPOPATIA..

Leave A Reply