The House of Favourite Newspapers

Mgombea Mwenza wa CCM Aendeleza Kampeni kwa Kishindo Njombe Mjini

0

Mgombea Mwenza wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, ameendelea na ziara ya kampeni mkoani Njombe ambapo amefanya mkutano mkubwa wa hadhara katika Halmashauri ya Mji wa Njombe tarehe 23 Septemba 2025.

Katika hotuba yake mbele ya maelfu ya wananchi waliojitokeza, Dkt. Nchimbi amewahimiza wakazi wa Njombe kuendelea kuiamini CCM kwa kuwa chama hicho kimeonesha uthabiti wa kuwaletea Watanzania maendeleo ya kweli katika sekta zote muhimu ikiwemo elimu, afya, miundombinu na ustawi wa kijamii.

Amesema kuwa Serikali ya CCM chini ya uongozi watakaounda itahakikisha inalinda misingi ya amani na mshikamano wa kitaifa huku ikiwapa kipaumbele vijana na wanawake katika ajira na fursa za kiuchumi.

Aidha, Dkt. Nchimbi ameahidi kuwa miradi ya kimkakati itakayotekelezwa katika awamu ijayo itaongeza thamani ya mazao ya kilimo na misitu, jambo ambalo litawanufaisha zaidi wakulima wa mkoa wa Njombe na kanda ya nyanda za juu kusini kwa ujumla.

Kwa upande wao, baadhi ya wananchi waliohudhuria mkutano huo wamesema wana imani kubwa na chama hicho kutokana na utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo barabara, hospitali na huduma za kijamii ambazo zimeboresha maisha yao kwa kiwango kikubwa.

Ziara ya kampeni ya Balozi Dkt. Nchimbi mkoani Njombe ni mwendelezo wa mikutano inayoendelea kufanyika maeneo mbalimbali nchini kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.

Leave A Reply