The House of Favourite Newspapers

Simulizi ya Kusisimua…. MKATABA – 3

0

ILIPOISHIA  JUMATANO

“Sina uhakika na hili jambo.”

“Usinitaje, mimi nimekuambia tu kama shoga yangu. Sisi wote ni wazazi.”

“Sawa.”

“Lakini jambo lingine linalowashtua zaidi watu ni tabia yake ya kujipenda kupita kiasi. Muda wote msafi, ananukia marashi, ananyoa vizuri, anavaa nguo nzuri…kwanini ajipende hivyo kama mtoto wa kike? Mchunguze mwanao shoga yangu!” 

SASA ENDELEA….

 

MAMA Suma alikuwa kimya kabisa, hakuwa na la kujibu, tayari walikuwa wameshaingia mtaani kwao. Mama Mwaija akaagana na mama Suma ambaye nyumbani kwake ilikuwa mtaa wa pili.

***

Siku nzima mama Suma alishinda na mawazo. Maneno aliyoambiwa na mama Mwaija yalimuumiza sana. Hayakuwa mambo mapya kwake, ila alishtuka baada ya kugundua kwamba kumbe yanajulikana na watu walishaanza kuyajadili!

 

Hata yeye mwenyewe alikuwa na mawazo sana juu ya tabia ya mwanaye kujipenda kupita kiasi. Jambo lingine lililomtesa ni kutokana na tabia yake ya kutopenda kabisa kuwa karibu na wanawake.

“Mwanangu jamani, hivi inawezekana ni kweli anafanya huo mchezo?” akawaza mama Suma.

“Lakini ngoja nitazungumza na baba yake, lazima nitafute ukweli wa hili jambo, ni aibu sana kwa familia yangu,” akaendelea kuwaza.

 

Jioni mumewe alivyorejea kutoka kazini, jambo la kwanza kuzungumza naye lilikuwa ni juu ya Suma.

“Kuna nini tena mke wangu?”

“Zungumza na mtoto, Suma anapotea.”

“Kivipi? Bado una yale mambo tu?”

“Siyo ninayo? Hata mtaani sasa wameanza kuyazungumza.”

“Mtaani?”

“Ndiyo.”

“Kivipi?”

 

Mama Suma akamsimulia mumewe kila kitu jinsi alivyozungumza na mama Mwaija. Baba Suma alishtuka sana, hakutegemea kama mwanaye angekuwa akisemwa hivyo mitaani.

“Ngoja nitakwenda kuzungumza naye.”

“Ndiyo maana alivyoamua kujitegemea amekwenda kupanga Majengo, hataki kukaa hapa mtaani kwa sababu wameshajua tabia yake.”

“Mke wangu acha kumhukumu mtoto kabla hujawa na uhakika, Jumapili nitakwenda kwake, nitajua huko huko.”

 

“Rajabu ameshaoa, Elibariki ana mchumba, Meshack ndoa yake ilikuwa Jumamosi iliyopita, wote hawa amemaliza nao shule, mbona yeye hana hata mtoto wa kusingiziwa mitaani? Lazima kuna kitu,” akasisitiza mama Suma.

“Nimesema nipe muda nikazungumze naye, ukweli utajulikana mke wangu,” akasema baba Suma.

“Sawa.”

***

 

Alichelewa sana kutoka kazini siku hiyo, tayari ilikuwa imeshatimu saa moja na dakika zake za jioni. Alikuwa amechoka sana lakini pia alikuwa na hamu ya kujua mengi zaidi kuhusu majini.

Alikuwa amesimama kwenye duka maarufu la viatu mjini Moshi liitwalo Bora, akakumbuka kwamba katika jengo lilelile kuna ukumbi wa sinema  wa Plaza. Asingeweza kwenda hadi Majengo akawahi kuangalia kwenye vibanda vya mitaani wakati ukumbi ulikuwa pale pale.

“Tatizo watakuwa na hiyo filamu?” akawaza.

“Ngoja nijaribu,” akajisemea.

 

Akapandisha juu haraka, ambapo alipita mbele ya duka la vifaa vya ujenzi la Njiwa Hardware, akapanda hadi kwenye ubao wa matangazo ya filamu katika Ukumbi wa Plaza Cinema.

Saa 12:00 jioni – Game in Forest (Billy Blanks)

Saa 2:00 usiku – Vampire’s With True Love (Sarafina Hollins)

Saa 4:00 – Shamba Kubwa – Kiswahili (Mzimuni Theatre Group)

 

Wengi walikuwa wakifurahia sana kuona kwamba kuna Filamu ya Shamba Kubwa ambayo ni ya Kiswahili. Ilikuwa filamu ya kwanza ya Kiswahili kuoneshwa katika ukumbi huo. Ingawa ratiba ilionesha kwamba ingeoneshwa saa 4:00 usiku, walikuwa tayari kusubiri!

Kwa Suma ilikuwa tofauti kabisa, alirukaruka juu kwa furaha alipoona Filamu ya Saa 2:00 usiku – Vampire’s With True Love, pamoja na elimu yake ya kawaida ya kidato cha nne, aliweza kupata tafsiri rahisi kuwa, sinema ile ilikuwa juu ya majini wenye upendo wa kweli.

“Haya ndiyo mambo ninayoyataka sasa,” akasema moyoni mwake kisha akatoka na kuvuka barabara.

Moja kwa moja aliingia kwenye Mgahawa wa Shaonaro kwa lengo la kupata chakula ili kuvuta muda wa kuingia kwenye sinema. Alikula kijeshi, robo saa kabla ya sinema kuanza tayari alikuwa dirishani akikata tiketi – alichosubiri ilikuwa ni muda tu!

 

Dakika zilikwenda taratibu sana, lakini hatimaye akaona watu walioingia saa 12 wakitoka, haraka akatupa macho yake kwenye saa yake ya mkononi, zilibaki dakika tano tu. Watu walipoisha, akaingia zake ukumbini na kukaa siti za mbele kabisa akisubiri muda ufike.

Saa 2:00!

Sinema ikaanza!

***

 

“Majengo Polisi….” sauti ya konda ilisikika akiuliza abiria wake.

“Shusha!” Suma akasema kwa sauti kubwa kwa kuwa alikuwa amekaa siti ya nyuma.

“Polisi?!!!”akauliza tena.

“Amesema shusha….tatizo nyie makonda huwa mnauliza abiria halafu mnatoa vichwa nje, mtasikiaje?” abiria mmoja akadakia.

“Tuliza mzuka, nimesikia.”

 

Daladala ile iliyotokea Mbuyuni kuelekea Kiboriloni ilisimama kwenye makutano ya barabara ya kuelekea Kituo cha Polisi Majengo. Suma akalipa nauli na kushuka zake, akavuka barabara na kuanza kutembea taratibu.

Akiwa anakaribia kufika Posta, akakutana na msichana mrembo sana. Alikuwa mweupe, mrefu, mwenye tabasamu pana, aliyevalia gauni aina ya dira. Suma alivutiwa naye sana, akamwangalia kwa muda mrefu sana bila kupepesa macho. Alivyokutana naye kabisa, akajifanya kuangalia pembeni.

Walivyopishana, Suma akageuza shingo; akakutana uso kwa uso na yule msichana. Alikuwa na tabasamu pana sana. Wote wakasimama.

“Si vibaya tukisalimiana,” yule msichana akasema akitabasamu.

 

Suma hakuwahi kupata mshtuko wa moyo kama wakati huo. Alihisi moyo wake kama umepigwa shoti ya umeme baada ya kusikia sauti tamu ya yule dada. Hakukumbuka kama hakumjibu ila naye aliendelea kutabasamu.

“Mambo vipi?” yule dada akasalimia.

“Poa, mzima?” akaitikia Suma.

“Wa afya.”

Wakapeana mikono.

“Mimi naitwa Zakhia, sijui mwenzangu?”

“Suma.”

“Unaishi mitaa gani?”

 

“Hapo chini, jirani na Makando Bar.”

“Sawa.”

“Wewe je?”

“Nakaa nyuma ya nyumba ya Kishamba Dispensary.”

“Ahsante, nimefurahi kukutana na wewe.”

“Hata mimi pia, ingawa nataka kukuambia jambo litakalokushangaza kidogo,” akasema Zakhia.

“Jambo gani hilo la kushangaza?”

“Samahani lakini, usinielewe vibaya.”

“Niambie.”

 

“Suma mimi ni mwanamke, najua sina haki ya kueleza hisia zangu kwa mwanaume kwa sababu wengi wanachukulia kama ni tabia mbaya, lakini naogopa kuacha kufanya hivi kwa muda huu maana sina uhakika wa kukutana tena na wewe…” akasema Zakhia kisha akatulia kwa muda.

Pumzi ndefu zilivutwa puani mwa Zakhia, kisha akaanza kuzishusha taratibu kabisa. Suma alikuwa kimya akimsikiliza. Alishahisi jambo lililokuwa njiani kumfikia…

“Hisia? Hisia gani hizo Zakhia?”

“Nakupenda sana!”

Suma akakunja uso.

“Samahani Suma, usinielewe vibaya tafadhali, ni hisia za moyo wangu. Nilijua ungenifikiria vibaya, lakini sina namna ya kuficha hisia hizi wakati ni kweli ninakupenda kutoka ndani ya moyo wangu.”

“Samahani sana Zakhia.”

“Niambie tu!”

 

“Wewe ni mwanamke mrembo sana, lakini hatuwezi kuwa wapenzi.”

“Kwanini?”

“Basi tu!”

“Au una mtu wako?”

“Sina.”

“Hujanipenda?”

“Hapana.”

“Bali tatizo ni nini sasa?”

“Tatizo ni msimamo wa maisha.”

“Unamaanisha nini?”

“Katika maisha yangu sijapanga kumuoa mwanamke na kumuoa.”

“Kwanini?”

“Ni utaratibu tu.”

 

“Kwahiyo hutaoa?”

“Hapana…natarajia kuoa lakini siyo bi….” Suma akakatiza sentesi yake baada ya kujisahau na kutoka kumponyoka neno ambalo hakutaka lisikike.

Zakhia akashtuka sana. Hakuelewa alichokuwa akimaanisha Suma. Haraka neno likamponyoka: “Sijakuelewa.”

“Samahani, kwaheri,” akasema Suma kwa sauti ya ukali kidogo kisha akaondoka zake.

“Watu wengine kwa kuingilia maisha ya wenzao bwana…sijui balaa gani hili?” akawaza kichwani mwake Suma.

Zakhia alibaki amesimama kwa mshangao akimsindikiza Suma kwa macho hadi alivyoishilia. Hakuwa na jibu sahihi juu ya yale yaliyotokea.

***

 

Mtu aliyekuwa akigonga mlangoni asubuhi hiyo ndiye aliyemshtua Suma usingizi. Ilikuwa Jumapili, saa 2:30 za asubuhi. Muda ambao kwa siku ya mapumziko kama hiyo huwa yupo kitandani hadi saa 4. Akatoka kitandani na kusogea hadi mlangoni, akafungua.

Alikuwa ni baba yake mzazi.

“Kumbe baba, karibu sana baba…” akasema Suma kwa furaha.

“Ahsante.”

“Shikamoo mzee.”

“Marhaba,” akaitikia akionekana hana furaha kabisa usoni mwake.

 

“Vipi baba, mbona kama haupo sawa? Kuna tatizo gani?”

“Tatizo lipo Suma mwanangu, tena tatizo kubwa sana lakini leo nahitaji hili tatizo liishe.”

“Ni nini baba?”

“Matusi tunayotukanwa sasa yanatosha. Njoro nzima inatutusi kwa sababu yako. Umetuvua nguo mwanetu.”

“Ni juu ya nini baba?”

“Wewe una tatizo gani?”

“Kuhusu nini baba?”

“Kwanini hutaki kuoa?”

“Ni hilo tu baba?”

“Kwani dogo?”

 

“Hapana mzazi wangu, nipe muda nijipange baba. Tatizo ni maisha hakuna kingine.”

“Unataka maisha gani zaidi ya haya?”

“Baba sina fedha, nitamtunza vipi mwanamke?”

“Mwanangu kila mtu huja na riziki yake. Kuoa ni faradhi, utajiwekea riziki mwenyewe mpaka utashangaa. Tafadhali nisikilize baba yako, mambo yanayozungumzwa kuhusu wewe ni makubwa sana, kikubwa ninachokuomba oa mwanangu. Kama huna mwanamke sema nikutafutie mimi mwenyewe, nimechoka na haya matusi ya mtaani.”

 

Suma alitulia kwa muda, akatafakari sana kisha akamwangalia baba yake…

“Nimekuelewa baba, nipe muda nitakuwa nimekamilisha hili suala.”

“Muda gani?”

“Miezi sita inatosha.”

“Mingi sana.”

“Baba ulichoniambia siyo chepesi kiasi hicho, ndiyo maana nimekuomba unipe miezi sita nitakuwa nimeshapata mtu sahihi.”

Baba yake akatingisha kichwa kukubaliana na jibu la mwanaye.

 

“Tafadhali na iwe hivyo.”

“Nakuahidi baba.”

“Sawa, ngoja mimi nikuache sasa.”

Suma akafungua droo la kabati la nguo, akatoa fedha kidogo na kumpatia baba yake. Hawakuwa na mazungumzo zaidi, mzee huyo akaondoka.

 

Kichwani mwa Suma kulikuwa na mwanamke mmoja tu; Zakhia! Ingawa hakutaka kuharibu mipango ya maisha yake, lakini aliona si vyema kuwaudhi wazazi wake, Zakhia ndiye mwanamke pekee ambaye angekidhi kuwa mke wake!

 

“Alisema anakaa kwa Kishamba….nitamfuatilia, tena leo hiihii!” akajisemea kwa sauti ya chini.

“Lakini pia sitakiwi kuacha wazo langu lipotee. Nitamfuatilia lakini wakati huo huo nitandelea kufikiria namna ya kupata jini wangu wa kuoa. Nimeshasikia maneno eti natakiwa kupuliza manukato makali chumbani, ngoja nitajaribu kufanya hivyo.

“Hapa inabidi nitumie mbinu mbili kwa wakati mmoja. Najua nitafanikiwa tu. Hawa wazee nao wananiingilia sana kwenye mambo yangu. Ngoja nitaona mwisho wake,” Suma akawaza.

Akajirudisha kitandani.

***

 

Aprili 14, 1996
Majengo, Moshi – Kilimanjaro

MOSHI nzima ilikuwa kimya kabisa, ni siku ambayo ilitawaliwa na mvua za rasharasha karibu siku nzima. Usiku wa kuamkia siku hiyo, mvua kubwa ilikesha, ilikatika alfajiri kabisa na kusababisha hali ya hewa kuwa tulivu sana.
Kwa namna udongo wa mji huo ulivyo, kila mahali kulikuwa na tope jingi kwenye barabara za mitaani. Ni kama vile mvua hiyo iliamua kuacha kunyesha ili kuwapisha waumini wa dini ya Kikristo waende kanisani.
Ilikuwa Jumapili ya Matawi, katikati ya Kipindi cha Kwaresma ikiwa ni wiki moja kabla ya Sikukuu ya Pasaka. Kuanzia saa nane mchana, mvua ikaanza tena kunyesha. Ilinyesha kwa saa moja kwa kasi ya ajabu, halafu ikakatika kisha ikafuata rasharasha.

Suma alikuwa ametulia kimya chumbani mwake. Alikuwa na mawazo mengi sana; kwanza alimfikiria baba yake na uamuzi wake wa kumtaka aoe haraka, halafu pili alikuwa akimfikiria msichana ambaye angalau anaonekana kufaa kuwa mkewe – Zakhia. Juu ya yote hayo, aliwaza zaidi namna ambavyo anakwenda kubadilisha nadhiri aliyojiwekea kwa muda mrefu sasa.

Alitamani sana kuoa jini na si binadamu. Kichwani mwake aliamini ni jini pekee ndiye ambaye angeweza kumfanya akaishi maisha ya raha mustarehe. Katika ubongo wake kulijengeka taswira ya kwamba majini ni viumbe wenye mapenzi, wasiotesa na wanaojali kuliko binadamu ambao wamekuwa wasaliti mara kwa mara kwa wenzi wao.
“Tatizo ni hilo…” akawaza.
“Lakini nitawezaje kujipinga mwenyewe?”

Alipata tabu sana ya kuwaza na kuwazua kichwani mwake. Akiwa mwenye kujiuliza maswali lukuki na kujijibu mwenyewe: “Mimi sina pesa, sasa msichana mzuri kama Zakhia, nitawezaje kumtunza na akaishi vizuri kama wanawake wengine? Jamani si nitadhalilika mimi? Au nikubali tu? Baba alisema kwamba kuoa ni jambo jema na mwanamke huja na riziki yake…
“Sasa kama aliniongopea nitajuaje?  Nitawezaje kufanya majaribio katika jambo makini na linalohusu maisha yangu kama hili? Nitaweza kweli? Lazima nipate jibu la swali hili kwanza. Sitakiwi kukurupuka tu….sitakiwi kabisa…mimi ni mwanaume mwenye akili timamu na kichwa changu kinafanya kazi vizuri.

“Mwanamke anahitaji matunzo. Nitayatoa wapi? Baba ananidanganya na maneno yake ya uongo mtupu…kama mwanamke huja na riziki yake, mbona yeye amemuoa mama na wametuzaa sisi hadi tunakuwa wakubwa, bado wanaishi maisha duni? Wanaishi nyumba ya kupanga? Au mama hana riziki? Sisi watoto wao je? Uongo mtupu!” aliwaza Suma.
Kwa kiasi kikubwa alipingana na mawazo ya baba yake, alijua ni ya kumshawishi tu! Hata hivyo, kuna jambo liliingia kichwani mwake kwa kasi ya ajabu sana. Alitakiwa kuheshimu na kusikiliza mawazo ya baba yake, lakini akiendelea kufanyia kazi ndoto zake.

“Acha nikazungumze na Zakhia, muda ambao nipo naye nitaendelea kufikiria namna ya kumpata jini wangu,” akawaza Suma.
Wazo hilo lilipita, tena aliamua kwenda kumfuatilia siku hiyohiyo. Tatizo likawa ni mvua. Aliendelea kusubiri sana mvua ipungue lakini haikukatika. Rasharasha ziliendelea. Hadi saa kumi mvua ilikuwa haijakatika. Alichoamua ilikuwa ni kutoka kwa kutumia mwavuli wake. Alipita njia za mkato.

Muda mfupi baadaye alikuwa anapita kwenye makutano ya barabara inayoelekea Faya na ile inayopandisha kwenda sokoni kupitia kwenye Baa ya Kipanga. Alikazana hadi alipokutana na Barabara ya Tunisia inayoelekea Mbuyuni kupitia Kiwanda cha Kahawa cha Coffee Quring na ile inayopandisha kwenda Kwa Kishamba.

Akashika ya kulia kwake. Hakuuachia mwavuli wake ambao ulimsaidia sana kuzuia mvua iliyoendelea kunyesha. Dakika tatu baadaye alikuwa ameshafika Kwa Kishamba.  Kama alivyoelekezwa na Zakhia, alizunguka nyuma ya Zahanati hiyo na kwenda kusimama kwenye duka moja mbele ya nyumba hiyo.

 

“Habari yako ndugu yangu?” Suma akamsalimia mhudumu aliyekuwa pale dukani.

“Salama, karibu.”

“Ahsante…sihitaji bidhaa yoyote dukani kwako ila naomba kuuliza.”

“Uliza tu ndugu yangu.”

“Kuna msichana namwulizia, alinielekeza anaishi humu ndani.”

“Anaitwa?”

“Zakhia.”

“Zakhia?” akamwuliza kwa mshangao kidogo.

“Vipi mbona umeshtuka ndugu yangu?”

 

“Ni ndugu yako?”

“Hapana ni rafiki yangu.”

“Dah!”

“Vipi kwani?”

“Yule matawi ya juu sana, nimeshangaa kuona mnafahamiana tena mna ukaribu.”

“Kawaida tu, yupo lakini?”

“Kwani yeye amekuelekeza lini hapa?”

“Muda kidogo, ni kama miezi minne hivi imepita.”

“Ni kweli alikuwa anaishi hapa…”

“Na sasa?”

 

“Amehama.”

“Amehamia wapi?”

“Soweto.”

“Dah….sijui itakuwaje sasa?” akasema kwa sauti Suma.

“Vipi ni muhimu sana kuonana naye?”

“Sana tena sana yaani.”

“Pole sana, unajua anapofanyia kazi?”

“Hapana.”

“Nitakusaidia, labda hapo unaweza kumpata.”

“Nitashukuru sana ndugu yangu.”

“Anafanya kazi Benki ya CRDB.”

 

“Wapi?”

“Ile iliyopo kwenye round about. Jengo la Kahawa.”

“Ahsante sana kaka, utakuwa umenisaidia sana. Ngoja nitajaribu kwenda kumwulizia pale.”

“Poa bwana.”

Suma akaondoka zake.

 

Kusoma hadithi zaidi za Joseph Shaluwa, tafadhali mfuate kwenye ukurasa wake wa Facebook: Simulizi za Joseph Shaluwa

ITAENDELEA KESHO JUMATATU….

Leave A Reply