The House of Favourite Newspapers
gunners X

Mlinda Mlango wa Nigeria, Stanley Nwabali Afiwa na Mama

0

Mlinda mlango shujaa wa Nigeria, Stanley Nwabali, amekumbwa na wingu zito la majonzi kufuatia kifo cha mama yake mzazi, aliyezikwa juzi yeye akiwepo, tukio ambalo limewasikitisha wapenzi wengi wa soka.

Katika hali ya kuumiza, Nwabali amefunguka kuwa pigo hili limekuja kama muendelezo wa mfululizo wa misiba, kwani alimpoteza bibi yake na kufuatiwa na baba yake ndani ya kipindi kifupi, na sasa mama yake amefariki ikiwa ni mwaka mmoja tu tangu matukio hayo ya awali.

Mchezaji huyo ameelezea kuwa dunia yake imesambaratika kabisa na anapitia maumivu makali ambayo hajawahi kuyadhani, huku akijaribu kutafuta nguvu ya kusimama tena baada ya kuondokewa na nguzo muhimu za familia yake.

​Picha za mazishi zimeonyesha mchezaji huyo akiwa katika hali ya simanzi kubwa, akishiriki taratibu za mwisho za kumhifadhi mama yake kwenye nyumba yake ya milele. Nwabali amemuelezea mama yake kuwa alikuwa mtu mwenye upendo, fadhili, na mkweli, na ameahidi kumkumbuka na kumpenda maisha yake yote.

Tukio hili limewagusa mashabiki na wadau wengi wa soka ambao wameendelea kutuma salamu za pole na faraja, wakimwombea mchezaji huyo apate nguvu na ujasiri wa kukabiliana na mapigo haya mazito yaliyoikumba familia yake ndani ya kipindi kifupi.

Hali hii ya Stanley Nwabali inatukumbusha upande wa kibinadamu wa wachezaji wetu mashuhuri, ambao licha ya kutupa furaha uwanjani, wanapitia majaribu mazito ya kimaisha. Dunia ya soka barani Afrika inaungana na nyota huyu katika kipindi hiki cha giza totoro, ikimuombea amani na faraja wakati akijaribu kuponya majeraha ya kuondokewa na watu wake wa karibu. Mungu aipe nguvu familia ya Nwabali na amlaze mama yake mahali pema peponi.

Stori na Elvan Stambuli, Global

Leave A Reply