The House of Favourite Newspapers

Muuaji Akosekana, DPP Afunga Jalada Mauaji ya Akwilina

MKURUGENZI wa Mashtaka nchini (DPP), Biswalo Mganga, amefunga rasmi jalada la kesi ya mauaji ya aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini na kuonya watu wanaovunja amani ya nchi kutofumbiwa macho wakiwamo waandishi wa habari.

 

Biswalo ameyasema hayo leo Aprili 20, 2018, Ikulu jijini Dar es Salaam alipozungumza na waandishi wa habari na kusema jeshi la polisi linapotumia nguvu kuzuia maandamano, haliwezi kushtakiwa.

 

”Katika maandamano hayo, kulikuwa na watu zaidi ya 200, huwezi kubaini ni nani aliyehusika kumpiga risasi Akwilina, lakini pia mwili wake haukutolewa risasi yoyote. Kama jalada nimelifunga, kwa hiyo askari waliotuhumiwa nao wameachiwa huru kwa maana hawana hatia,” alisema Biswalo.

 

Biswalo amesema miongoni mwa majukumu yake ni kuhakikisha amani inakuwapo, “mimi sina chama cha siasa, si mwanasiasa, sitamvumilia mtu awe mkubwa wala mdogo, nitamshughulikia.

 

“Wanaosema wataandamana, waambieni wasifanye hivyo, wakiandamana watakwenda kuwasimulia familia zao,” amesisitiza Biswalo.

Biswalo amevitahadharisha vyombo vya habari vinavyoweza kuchangia uvunjifu wa amani ya nchi na kusema hatua zitachukuliwa, amevitaka viwe makini na kutimiza wajibu wao kwa kufuata misingi ya taaluma yao ya habari.

Comments are closed.